Header Ads Widget

MILIONI 61/= ZATENGWA KUKAMILISHA UJENZI WA SHULE YA MAPITA

 


NA JOSEA SINKALA, MBEYA.


Wanafunzi wa shule ya msingi katika kijiji cha Mapita kata ya Izyira Mbeya vijijini, hutembea umbali mrefu kufuata huduma ya haki elimu katika vijiji vingine kutokana na kijiji chao kutokuwa na shule ya msingi.


Wakizungumza na Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza, wananchi wa kijiji hicho wamesema walianza jitihada za kujenga shule na kujenga zaidi ya majengo matano lakini moja lilibomolewa na mvua za msimu uliopita.


Dickson Mdonyela ni mkazi wa kijiji cha Mapita, anasema "Mimi nimefanya jitihada za kuhakikisha tunaungana kujenga shule kulingana na miundombinu ya barabara huku kwetu, kweli barabara ni kero hasa kifuku japo tunashukuru mmekwangua barabara lakini kifuku hazipitiki kwahiyo watoto inakuwa vigumu kufika shuleni hivyo tunaomba shule ikamilike hapa kijijini kwetu (Mapita)", ameeleza mwananchi huyu.


Kwa mujibu wa uongozi wa Serikali ya kijiji cha Mapita, wananchi wanaendelea na ujenzi wa majengo ya shule ya msingi Mapita kwa nguvu zao wakitumia ushauri wa wataalam wa ujenzi kutoka Halmashauri ya Mbeya.


Kaimu afisa elimu msingi wa Halmashauri ya Mbeya Fabian Mtisi, amesema kwa kutambua kijiji hicho kutokuwa na shule ya msingi, tayari Serikali kupitia mradi wa Boost imetenga fedha kiasi cha shilingi million sitini na moja kwa ajili ya ukamilishaji shule hiyo ya msingi.


"Mheshimiwa Mbunge (Oran Njeza) na ndugu wananchi, kwa kutambua hilo tayari Serikali imetenga million sitini na moja kupitia mradi wetu wa Boost ili kuja kuunga mkono juhudi za wananchi hawa wa kijiji cha Mapita niwaombe kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mbeya kwamba endeleeni na kuandaa vitu vingine kama tofali tuwe na benki ya tofali hapa ili fedha hizi zitakapoingizwa kwenye akaunti ya shule mama ya Izyira basi tukakamilishe ujenzi na kuisajili haraka sana", ameeleza Afisa elimu msingi Halmashauri ya Mbeya.


Afisa elimu huyo amewaomba wananchi kuendelea kujitoa kuandaa miundombinu mingine ili fedha zitakapoingia shule hiyo ikamilike na kusajiliwa mapema iwezekanavyo.



Naye Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza, amewashukuru wananchi wake kwa kuwa na moyo wa kujitoa na kupenda maendeleo akiahidi kushirikiana nao kuhakikisha shule yao inakamilika na kusajiliwa ili kuwaepusha watoto na kadhia ya kutembea umbali mrefu kufuata elimu katika vijiji vya Inuka, Masewe na Izyira.


"Mkurugenzi ukiangalia kwa umakini utagundua wananchi kwenye taarifa yao hawajasema kero nyingine hapa zaidi ya shule. Barabara imechongwa, umeme umefika, maji mradi unakuja Izyira hapa kwahiyo kilio cha wananchi hawa namimi naungana nao ni shule, mimi niwahakikishie niko pamoja na ninyi na nitahakikisha shule inakamilika na inasajiliwa. Uzuri na mfuko wa jimbo nimeshachangia hapa kwahiyo asiwadanganye mtu elimu ndio kila kitu katika Dunia ya sasa na ijayo bila elimu ni sawa na bure", ameeleza Mbunge Oran Njeza wa Mbeya vijijini.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI