Na Thobias Mwanakatwe,IRAMBA
KAMPUNI ya Biosustain Tanzania Limited imekabidhi bweni la kisasa walilojenga katika Shule ya Sekondari Mtekente iliyopo wilayani Iramba mkoani Singida kwa viongozi wa kata ambalo limejenga kwa Sh.milioni 180 kwa kushirikiana na Cotton Made in Africa.
Kampuni hiyo ambayo inamiliki kiwanda cha kuchambua pamba kilichopo Manispaa ya Singida mbali na kujenga bweni hilo pia imejenga jiko la shule,kisima cha maji na imenunua vitanda na magodoro kwa ajili ya wanafunzi wa shule ambapo mradi huo ulikabidhiwa rasmi jana kwa viongozi wa kata ya Mtekente hiyo wakiongozwa na Diwani wa kata hiyo,Noel Shole.
Meneja Miradi wa Biosustain Tanzania Limited, Tawanda Mutonhori, akikabidhi mradi huo, alisema kampuni hiyo kwa kushirikiana na Cotton Made in Africa (CmiA) ya nchini Ujerumani wametekeleza mradi huo ikiwa ni sehemu ya kuunga juhudi za serikali za kumuinua mtoto wa kike kielimu.
Alisema walilazimika kujenga bweni hilo kutokana na changamoto wanazopitia wanafunzi wa kike wa shule hiyo kwa kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani kwenda shule huku wengine wakipanga mitaani hali iliyokuwa ikisababisha utoro na wengine kukata tamaa na kuacha shule.
"Kampuni imeweza kujenga bweni lenye uwezo wa kubeba wasichana 80, vitanda 40 (double deck),magodoro na pia imejenga jiko kwa ajili ya kupikia chakula,mabafu ya kisasa 10 yenye sehemu ya kufulia,imechimba kisima cha maji chenye uwezo wa kutoa maji lita 5,000 kwa saa moja na kujenga mnara wenye tanki la maji linalobeba lita 10,000," alisema.
Naye Diwani wa Kata ya Mtekente, Shole akizungumza baada ya kukabidhiwa mradi huo aliishukuru kampuni ya Biosustain Tanzania Ltd na Cotton Made in Africa kwa mchango wao mkubwa kusaidia kuboresha sekta elimu katika kata hiyo.
"Biosustain wamefanya jambo kubwa katika kata yetu ombi langu kwenu wananchi Biosustain anajishughulisha na kilimo cha pamba na ununuzi wa pamba hivyo twendeni tukawaunge mkono kampuni hii kwa kulima pamba kwa wingi katika kata yetu kwani pamba ni dhahabu nyeupe," alisema.
Shole alisema ili kufikia malengo ya kulima pamba kwa wingi alimwagiza Afisa Kilimo kata ya Mtekente kuanza mikakati ya kuwahamasisha wananchi kulima pamba kwa kufahya mikutano kwa kila kijiji na kitongoji.
"Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtekente nakuagiza katika msimu huu unaoanza wa 2024/2025 shule ilime ekari tano za pamba, na mimi nitafanya ukaguzi kwa viongozi wote wa kata kuhakikisha kila mmoja analima pamba lengo ni kuongeza uzalishaji wa zao hilo," alisema.
Shole alisema wananchi wanapaswa kuiunga mkono kampuni ya Biosustain kwasababu wanafanya kazi katika mikoa mitatu lakini wamefanya upendeleo katika kata hiyo kwa kujenga bweni,jiko na kuchimba kisima cha maji katika shule ya sekondari Mtekente.
Diwani huyo aliwataka wazazi ambao watoto wao watachaguliwa kwenda bwenini wafanye hivyo na kusiwe na visingizo kwamba kuna mapepo.
"Watoto watakaochaguliwa kwenda hosteli waje wakaishi huko kweli sio habari ya mtoto kuja kuchaguliwa halafu mzazi unaanza kusema kule kuna mapepo,mapepo umeyaleta wewe," alisema Shole.
Diwani huyo alisema wananchi hawanabudi kuiunga mkono kampuni ya Biosustain kwa kulima pamba kwa wingi na hiyo ndio itakuwa zawadi kubwa kwao hali itakayoifanya kampuni hiyo kuwa na ari ya kusaidia katika miradi mingine ya maendeleo katika kata hiyo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtekente,Nivard Ngokotalo,alisema ujenzi wa bweni hilo utaondoa changamoto ya utoro kwa wanafunzi ambao walikuwa wanatembea umbali mrefu haku iliyokuwa inawaathiri kimasomo.
"Tunaishuruku kampuni ya Biosustain Tanzania Ltd kwa mradi huu wa bweni kwani wametusaidia kuounguza tatizo la utoro kwa wanafunzi ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu hali hii itaongeza ari ya wanafunzi kusoma kwa bidii kwakuwa sasa watakuwa hawatembei muda mrefu," alisema.
Alisema shule hiyo ambayo ilianzishwa 2007 ina jumla ya wanafunzi 312 kati yao wasichana ni 156 na wavulana ni 156 na kwamba mpango uliopo kujenga bweni jingine kwa ajili ya wanafunzi wa kiume.
Naye Mtendaji wa Kata ya Mtekente, Festo Nicodem, alisema uongozi wa shule wahakikishe mazingira ya bweni hilo yanatunzwa vizuri kusiwe na uharibifu.
Nicodemu alisema ujio wa bweni hilo utasaidia kupunguza utoro kwa wanafunzi hali ambayo ilikuwa ikiwapa changamoto viongozi hususani yeye Mtendaji ambaye ni mlinzi wa amani wa kata kuwatafuta wanafunzi watoro shuleni.
"Biosustain kimsingi wametukomboa sana na bila shaka kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kike kitaongezeka," alisema Mtendaji huyo wa kata.
Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Mtekente,Bahati Hussein alisema CCM inaipongeza Kampuni ya Biosustain Tanzania Ltd kwa kujenga mabweni hayo ambayo itakuwa ni mkombozi sana kwa wanafunzi hususani wa kike.
Bahati aliomba kampuni hiyo ikiwezekana mwakani wasaidie na ujenzi wa nyumba ya matroni ambaye atakuwa analea wanafunzi watakaokuwa bwenini.
Mhandisi kutoka Biosustain Tanzania Ltd,Rajabu Kandira, alisema bweni,jiko na kisima cha maji vimejengwa kwa kiwango bora kabisa ambapo kwa upande wa vyoo wamezingatia hata kwa watu wenye ulemavu.
0 Comments