NA JOSEA SINKALA, MBOZI SONGWE.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema pamoja na utajiri ulioko nchini lakini bado wananchi wake wanaendelea kuteseka na ufukara kutokana na mfumo mbovu wa Serikali katika kuweka mazingira rafiki ya wananchi kuishi.
Hayo yameelezwa na Mjumbe wa kamati kuu ya CHADEMA Taifa John Heche wakati akihutubia maelfu ya wananchi na wanachama wa Chama hicho kwenye mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Mlowo Jimbo la Mbozi mkoani Songwe.
Akiwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo, Heche amehutubia wananchi katika mji huo wa wafanyabiashara na wakulima akiiangukia Serikali kuendekeza anachokiita anasa kwa kununua magari ya kifahari ya viongozi huku huduma zikiwa mbovu kwa walipa kodi.
Heche anasema Tanzania ni tajiri kwa kuwa na raslimali mbalimbali ilizibarikiwa na Mungu ikiwemo mbuga za wanyama, maziwa, bahari, Bandari, madini aina mbalimbali, misitu na mali nyingine nyingi lakini kutokana na uongozi mbovu mali hizo hazina tija yoyote kwa wananchi badala yake baadhi zinakabidhiwa kwa wageni bila kuwafanya wananchi kuendelea kuwa na maisha magumu.
Mjumbe huyo wa CHADEMA Taifa anasema dawa ni kufanya mabadiliko kwenye chaguzi zijazo kwa kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za mitaa vitongoji na vijiji wananchi wanajiandikisha na kwenda kuichagua CHADEMA akidai endapo itashindwa kuleta mabadiliko ndani ya kipindi cha miaka mitano wakaitoe madarakani.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa Frank George Mwakajoka, amesema mabadiliko ya kweli yataletwa na CHADEMA itakapochaguliwa kuanzia Serikali za mitaa vitongoji na vijiji huku akikataa mfumo wa kuwa na viongozi wa kupita bila kupingwa.
Kiongozi huyo ametuma ujumbe kwa Serikali pamoja na Chama Cha Mapinduzi mkoani Songwe kwa kuandaa vijana (Green guard) kwa ajili ya kufanya fujo na kwamba wanawanyanyasa wananchi majira ya usiku kwa kigezo kuwa wanafanya mazoezi.
Naye mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Songwe Isakwisa Thobias Lupembe ameeleza kukerwa na kuendekezwa matendo ya ukatili na utekwaji wa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Pia amewaomba wananchi kwenda kuchagua viongozi bora kupitia CHADEMA kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwakani ili kuwatumikia wananchi kwa moyo wa kweli lasivyo anadai mazingira yataendelea kuwa magumu kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye biashara na kilimo.
Aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Mbozi na mtia nia ya ubunge jimboni humo ambaye pia ni mwenyekiti wa CHADEMA Digital Kanda ya Nyasa Pascal Yohana Haonga ameeleza kilio chake kwa Serikali kuwa na utitiri wa kodi na tozo kwenye kilimo hali inayodumaza sekta ya kilimo nchini ikiwemo kahawa inayolimwa kwa wingi jimboni kwake huku pia akikerwa na mfumo wa stakabadhi ghalani mfumo unaodaiwa kuwa kikwazo kwa wakulima.
Viongozi mbalimbali wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wa jimbo la Mbeya vijijini Getruda Japhet Lengesela, Mwenyekiti wa BAWACHA mkoa wa Songwe Bi. Agness Chilulumo, Mch. Amoni Mwashitete Mwenyekiti wa Chama hicho jimbo la Vwawa wamehudhuria mkutano huo wa hadhara katika mji huo wenye shughuli nyingi za biashara na kilimo na kueleza kero lukuki zinazowakabili wananchi na kuonyesha haja ya kufanya mabadiliko kwenye chaguzi zijazo ili kuwa na viongozi wanaodaiwa kuwa wawakilishi wa wananchi kwa maslahi ya umma na kwa maendeleo ya Taifa huku raslimali za Taifa zikilindwa na kuleta manufaa kwa wananchi wake badala ya kusalia kama watumwa kwenye nchi yao..
0 Comments