Gari lililokuwa limewabeba mashabiki 25 wa Yanga, tawi la Mwanza Mjini imepata ajali eneo la Chidingo, Mji Mdogo wa Katoro mkoani Geita, baada ya kugongana na pikipiki maarufu bodaboda.
Ajali hiyo imesababisha kifo cha dereva wa pikipiki hiyo, huku mashabiki wa Yanga wakinusurika na kuendelea na safari yao kurejea Mwanza.
Mashabiki hao walikuwa wakirejea jijini Mwanza baada ya kushuhudia mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Kagera Sugar, uliochezwa jana Agosti 29, 2024, kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.
Katika mchezo huo, Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Maxi Nzengeli na Clement Mzize.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo leo Ijumaa Agosti 30, 2024 ambapo ameeleza kuwa dereva wa bodaboda alifariki muda mfupi baada ya ajali kutokea huku akitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendesha pikipiki aliyekuwa akijaribu kulipita gari la abiria lililokuwa limesimama na hatimaye kugongana uso kwa uso na gari lililokuwa limebeba mashabiki wa Yanga.
Katibu wa tawi la Yanga Mwanza Mjini, Edson Cole, ambaye alikuwa sehemu ya msafara huo, amethibitisha kuwa mashabiki wote 25, wako salama.
Chanzo :mwananchi
0 Comments