Na Fadhili Abdallah,Kigoma
KIONGOZI wa Chama Mstaafu wa Chama Cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe amesema kuwa bado rasilimali za nchi zilizopo hazijaweza kutumika vyema kuondoa umasikini wa watanzania kutokana na baadhi ya viongozi kutokuwa na nia ya dhati ya kuwaondolea Watanzania hao umasikini hivyo mabadiliko ya uongozi hayana budi kufanyika sasa.
Kabwe alisema hayo akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika njia panda Simbo Halmashauri ya wilaya Kigoma akiwa kwenye siku yake ya pili ya ziara ya siku nane mkoani Kigoma ambapo alisema kuwa sera mbovu za CCM ndiyo imekuwa kikwazo kikubwa katika kufikiwa kwa maendeleo ya Watanzania.
Alisema kuwa viongozi wa Chama cha ACT wana nia ya dhati katika kuwatumikia na kuwaletea Watanzania maendeleo na ndiyo maana wanalo baraza kivuli la mawaziri ambalo linawasumbua mawaziri waliopo madarakani wanaotokana na CCM ili watekeleze matakwa ya Watanzania katika kuwatelea maendeleo.
Kiongozi wa Chama huyo Mstaafu alisema kuwa wanazo sera nzuri ambazo zinalenga kutengeneza ajira na kuongeza kipato cha mtanzania ili kuwaondoa watanzania kwenye lindi la umasikini hivyo ametaka wananchi wote kujiandikishwa kwenye mfumo wa ACT Kiganjani kuwa wanachama wa chama hicho sambamba na kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
“Mkoa Kigoma hauna sababu ya watu wake kuwa masikini mbegu ya Chikichi ilitoka Kigoma Kwenda Malaysia ambao kwa sasa wanazalisha mafuta ya mawese na kuiuzia dunia,lakini Kigoma wanayo ardhi ya kutosha, mvua ya kutosha na ardhi yenye rutuba lakini bado wanaandamwa na lindi la umasikini kwa sababu ya viongozi wake kukosa maarifa,”Alisema Kiongozi huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa ACT Wazalendo mkoa Kigoma,Kiza Mayeye alisema kuwa Zaidi ya miaka 60 ya kutawala Tanzania bado hali ya Watanzania wengi na mbaya kiuchumi na kwamba sera mbovu na zisizozingatia mahitaji ya watu wake ndiyo imewafanya Watanzania kufikia hapo walipo.
Pamoja na hilo Mwenyekiti huyo wa ACT mkoa Kigoma amelalamikia utiriri wa mageti ya polisi na uhamiaji barabarani ambayo yamekuwa yakiwasumbua wananchi lakini pia yamekuwa yakitumika kama chanzo cha rushwa na kuwabambikia wananchi kesi.
Mwisho.
0 Comments