Header Ads Widget

TK MOVEMENT YAZINDULIWA SINGIDA,VIJANA WAPEWA WITO KULINDA TUNU ZA TAIFA

 






"


Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA

MTANDAO wa Vijana na Wanawake ujulikanao TK Movement wenye lengo la kuendesha vuguvugu la kujitolea ili kuleta mapinduzi ya kifikra kwa jamii na kuhimiza kushiriki kwenye fursa umezinduliwa mkoani Singida huku vijana wakipewa wito wa kulinda tunu za taifa ambazo ni amani, utulivu na uzalendo.

Uzinduzi huo umefanyika jana (Julai 20, 2024)  mjini Singida na kushirikisha maelfu ya vijana na wanawake kutoka wilaya zote za Mkoa wa Singida ambao kabla ya kuzinduliwa walifanya maandamano kuzunguka mitaa ya mji wa Singiga yakiongoza na viongozi wa kitaifa na mkoa wa TK Movement.

Mkuu wa Mkoa wa Singida,Halima Dendego,ambaye aliwakirishwa na Mkuu wa Wilaya ya Singida,Godwin Gondwe, akizindua mtandao huo aliwataka vijana kuendelea kulinda tunu za taifa ambazo ni amani,utulivu na uzalendo ili nchi yetu iendelee kuwa na amani.

"Nchi yetu ina amani sana ndio maana mtu akienda dukani kununua kitu anasema naomba wakati anatoa hela yake,kwa hiyo wananchi wafahamu kuwa tunu za taifa ni mambo muhimu ya kujivunia kwa jamii yetu,tunu ndio msingi wa maadili na utamaduni wa jamii,"alisema Gondwe. 

Aidha, alisema vijana na wanawake kupitia TK Movement wanao wajibu kutangaza maendeleo makubwa yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan  ili wananchi wafahamu na hivyo kuendelea kuunga mkono na kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi inayotekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini.

Naye Mshauri wa TK Movement Taifa, Hemed Ali, alisema kutokana na Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 vijana na wanawake wapo zaidi ya asilimia 70 hivyo ni kundi muhimu katika maamuzi,ujenzi wa jamii bora na maendeleo ya  Taifa.

Ali alisema kwa kipindi kirefu vijana na wanawake wamekosa 'platform ' ya kukutana bila kujali itikadi za siasa, dini na ukanda lakini sasa kupitia TK Movement wataweza kukutana kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo yakiwemo upatikanaji wa fursa ambazo zitachangamkiwa na makundi hayo kuzipata.

"Ni wajibu sasa wa serikali na taasisi binafsi ziunganishe vijana na wanawake kuwapatia fursa zinazopatikana ili na wao waweze kushiriki vyema katika ujenzi wa uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla," alisema Ali.

Awali Mratibu wa TK Movement Mkoa wa Singida,Sophia Jumbe, alisema misingi ya mtandao huo ni utaifa,uzalendo na kujitolea ambapo mtandao utaendelea kuwaelimisha vijana wa kitanzania wawe na ufahamu mzuri wa mambo hayo ili wawe raia wema na kuchangia kwa njia chanya maendeleo ya nchi kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

"Tunaamini kwamba vijana wenye kuelewa na kuheshimu tunu za taifa ,uzalendo na kujitolea ndio watakaoivusha Taifa kuelekea kwenye kesho iliyo bora kuliko jana na leo hii ni kwasababu vijana ndio nguvu kazi kubwa ya taifa hili," alisema.

Sophia alisema kwa kutambua idadi kubwa ya vijana nchini na hatma ya nchi yetu kuwa iko mikononi mwao,mtandao wa vijana wa Taifa Letu,Kesho Yetu uliamua kuchagua misingi mikuu ya utahfa ,uzalendo na kujitolea kwa kuwa ndio tunu zitakazosaidia kuwa na taifa lenye umoja na mshikamano.

"Imani yetu ni kwamba ikiwa vijana wataelewa historia ya taifa lao na kuona fahari kwa sehemu ya taifa na ikiwa wataipe da nchi yao na kuwa tayari kujitolea kuitumikia nchi yao kwa vyovyote vile watafanya kazi kwa kujituma,watakuwa waadilifu na waaminifu katika shughuli mbalimbali watakazokuwa wanafanya," alisema.

Aliongeza kuwa idadi ya vijana wahitimu wa elimu ya juu wanaoingia soko la ajira ni 800,000 hadi 1,000,000 kila mwaka lakini wanaobahatika kupata ajira rasmi ni 40,000 sawa na asilimia 5 7 tu na hivyo asilimia 94.3 wanabaki mitaani kujishughulisha na mambo mengine ambayo hawakuyasomea.

"Kama hali ya ajira ni mbaya kiasi hiki kwa vijana wenye elimu na ujuzi bila shaka hali ni mbaya zaidi kwa vijana ambao hawakubahatika kupata elimu ya juu, tunatambua serikali haina uwezo wa kuajiri vijana wote ni kwa msingi huo tumeamua kuanzisha mtandao huu ili kuisaidia serikali kutoa elimu,mafunzo na hamasa kwa vijana," alisema.

Aliongeza kuwa serikali chinj ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipambanua kukuza uchumi wa nchi kwa kutanua wigo wa fursa za kiuchumi kwa kuongeza bajeti za miradi ya maendeleo kwa kila sekta kwa miaka minne mfululizo tangu iingie madarakani.

"Kwasababu hiyo tumeamua kumuunga mkono mheshimiwa rais kumnadi na kumwongezea ushawishi kwa kuzielezea kwa ufasaha na kwa takwimu kazi anazozifanya kupitia serikali yake ili wananchi waelewe vizuri na hatumaye wamchague tena kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa 2025," alisema Sophia.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI