Header Ads Widget

SOS ARUSHA YATOA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI KWA VIJANA 300 MKOANI ARUSHA.



Na,Jusline Marco;Arusha 


Shirika SOS Children Village la jijini Arusha kupitia Shirika la kuhudumia viwanda vidogo SIDO limeendesha mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana na walezi wa watoto takribani 300 wa  Mkoani Arusha.


Katibu Tawala Msaidizi anayehusika na Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mkoa wa Arusha Frank Mbando wakati akifungua mafunzo hayo amesema lengo ni kuwawezesha walezi na vijana kujikwamua kiuchumi na kuwa na uwezo wa kuwatunza na kuwalea watoto walio majumbani mwao.


Aidha amesema mafunzo hayo yatahusisha usindikaji wa vyakula mbalimbali ,utengenezaji wa bidhaa mbalimbali kama sabuni na nguo aina ya batiki ili waweze kujiingizia kipato na kukomboa familia zao.


Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita imeendelea kuweka msukumo wa kipekee kwa vijana,wanawake na makundi maalum ili kujikwamua kiuchumi kupitia vikundi mbalimbali ambapo amesema hadi sasa ipo mifuko na programu 84 zinazosaidia makundi mbalimbali kujikwamua kiuchumi.


"Niwatie moyo tu vijana kuchangamkia fursa hii, kama mnavyofahamu mkoa wetu huu ni mkoa wa kipekee ambao ndiyo kitovu cha utalii nchini na kinara ya diplomasia ya kiuchumi."alisisitiza Frank Mbando Katibu Tawala Msaidizi anayehusika na Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mkoa wa Arusha 


Naye Mratibu wa Uwezeshaji familia na Vijana kutoka Shirika la SOS Children Village Willson Rando amesema tangu kuanzishwa kwa mradi wa miaka 5 wa Arusha Reinovation mwaka 2022 lengo lilikuwa ni kuwafikia vijana 1000 na familia 1000 katika maeneo ya uwezeshwaji kiuchumi pamoja na mafunzo ya malezi kwenye jamii.


Amesema mradi huo unafanya kazi katika kulenga kuanzisha mifumo ya malezi mbadala kwenye jamii, kusaidia vijana kujikwamua kiuchumi pamoja na utoaji wa mafunzo ya ujasiriamali sambamba na kuwaonganisha katika fursa zinazoweza kupatikana kwenye ngazi ya halmashauri.


"Tunaamini tukiziwezesha hizi familia kwenye eneo la ujasiliamali zitaenda kusaidia kwenye kuboresha malezi ya watoto, na sasa hivi tunatoka kwenye kuwalea watoto ndani ya vijiji na tunaenda kutoa huduma kwenye jamii moja kwa moja".Alieleza Mratibu huyo


Kwa upande wake Meneja wa SIDO Mkoa wa Arusha Jalphary Donge amelishukuru shirika la SOS kwa hatua waliyoifikia katika mradi huo  kwa kuwafikia vijana kwenye maeneo wanayoishi ambapo mategemeo yao ni kuona uwezeshaji unaotolewa kupitia mafunzo yanayopatikana kupitia SIDO.

 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI