Header Ads Widget

MNZAVA-MFUMO WA NeST UNALETA UWAZI, UWAJIBIKALI NA KUONDOA MALALAMIKO YA WAZABUNI

 

Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA 

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2024,Godfrey Mnzava, amesisitiza  taasisi za umma kuendelea kuzingatia Mfumo wa Ununuzi wa Umma (NeST ) wakati wa kufanya manunuzi ili kuweka uwazi na uwajibikaji.



Amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Singida leo (Julai 8, 2024) baada ya Mwenge wa Uhuru kukagua barabara ya Minga yenye urefu wa kilometa 1.21 iliyojengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Sh. 992,096,092.




Mnzava amesema Rais Samia Suluhu Hassani ameendelea kuelekeza manunuzi ya umma yapitie katika mfumo wa Nest ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) lengo ni kuendelea kuweka uwazi,uwajibikaji na kudhibiti manunuzi ya umma.



Amesema kupitia mfumo huo wazabuni mbalimbali wanaomba zabuni moja kwa noja na kujua nani mwenye sifa na nani hana sifa na huu ni mkakati wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha kunakuwa na udhibiti katika manunuzi.



"Kumekuwa na malalamiko kwamba kuna watu wanapendelewa kupewa zabuni lakini kupitia mfumo wa NeST hakuna cha upendeleo kwani unaona kitu gani umekikidhi na kipi haujakidhi," amesema Mnzava.


Aidha,Mnzava ameipongeza Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) Manispaa ya Singida kwa kuzingatia mfumo wa NeST ambayo ndio maelekezo ya serikali katika suala la manunuzi.


Awali  Meneja wa TARURA Manispaa ya Singida,

Mhandisi Lazaro  Kitomari amesema ujenzi wa barabara ya Minga kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 1.21 inajengwa kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara ikiwa ni sehemu ya fedha inayotolewa kila mwaka kwa ajili ya matengenezo ya barabara. 


Amesema Wakala wa barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) ilipanga kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami katika awamu tatu,awamu ya kwanza ilijenga kilometa  0.6 katika mwaka wa fedha 2021-2022, awamu ya pili ilijenga kilometa  0.61 mwaka wa fedha 2022-2023 na  awamu ya tatu mwaka wa fedha 2023/2024  ambapo TARURA imefunga taa za barabarani 37.


Kitomari amesema gharama za mradi huu ni Sh.  344,128,092 awamu ya kwanza na Sh. 452,268,000 awamu ya pili mwaka wa fedha 2022-2023.


Awamu ya tatu ambayo imetekelezwa na Mkandarasi OTONDE CONSTRUCTION & GENERAL SUPPLIES LTD wa Mwanza kwa  Sh. 195,700,000 na hivyo ujenzi katika awamu zote tatu kufikia Sh. 992,096,092.


Ameongeza kuwa faida za barabara hii ni kupunguza gharama za uendeshaji vifaa vya usafiri, kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji, kupunguza vumbi/uchafuzi wa mazingira na kupendezesha mji, kupunguza gharama ya ukarabati wa barabara ya mara kwa mara na kuongeza usalama wa watumia barabara.


MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI