Header Ads Widget

CHADEMA RUNGWE YAAHIDI KUKOMBOA MAJIMBO YA BUSOKELO, RUNGWE







NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya kimewataka wananchi katika jimbo la Busokelo wilayani humo kuichagua CHADEMA kwenye chaguzi zijazo kwa madai kuwa chama hicho ndio tumaini la kweli kwa sasa.


Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Rungwe Paulo Said Zambi wakati akizungumza na viongozi wa CHADEMA jimbo la Busokelo kwenye kikao cha mashauriano jimbo pamoja na kamati tendaji ya wilaya yake.


Zambi amesema lengo la ziara yake katika jimbo la Busokelo ni kuona hali halisi ya maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa na kuhimiza maandalizi hayo ili kuhakikisha Chama chake kinachaguliwa.


Amesema Chama Cha Mapinduzi CCM kimeongoza kwa muda mrefu ikiwemo kwenye jimbo la Busokelo lakini wananchi waliobarikiwa raslimali mbalimbali bado wanakabiliwa na kero lukuki hivyo kuwataka viongozi kwenda kufanya mikutano ili kuwaambia wananchi umuhimu wa kuichagua CHADEMA kwenye Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwakani.


Kwa upande wake mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Busokelo Ande Kyamba, amesema kamati yake imefanya ziara katika kata mbalimbali na kuendelea kuandaa wagombea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa isipokuwa kata mbili ambazo bado hazijafanikiwa kuandaa wagombea.


Mwenyekiti huyo katika mahojiano na kituo hiki amesema watahakikisha wanatwaa nafasi nyingi za vitongoji na vijiji na kwa uchaguzi mkuu CHADEMA imedhamiria kumwondoa madarakani kupitia sanduku la kura Mbunge wa jimbo hilo Mhe. Atupele Fredy Mwakibete ili wananchi wapate mwakilishi sahihi.


Viongozi kutoka kata mbalimbali pamoja na mabaraza huko Busokelo, wanasema wanaendelea kujinoa kuhakikisha uchaguzi ujao wanashinda ili kuleta uwajibikaji wa viongozi na maendeleo kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI