Header Ads Widget

MITAA 9 YAANZA KAMPENI YA USAFI NJOMBE



Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE


Mamia ya wakazi wa mtaa wa Idundilanga kata ya Njombe mjini Mkoani Njombe wamejitokeza kushiriki zoezi la usafi ili kuweka mazingira katika hali ya usafi na kuepukana na magonjwa ya mlipuko.



Mapema asubuhi zoezi la usafi limeanza kwa kufunga maduka na ofisi zote ili kutekeleza azma ya serikali ya kuweka mazingira katika hali ya usafi.


Kata ya Njombe mjini imezindua rasmi kampeni ya usafi itakayodumu kwa siku 10 katika mitaa 9 huku uzinduzi ukifanyika katika mtaa wa Idundilanga ambapo Ofisa mtendaji wa kata hiyo Enocy Lupimo anasema yeyote atakaye kaidi atapigwa faini ya shilingi elfu 50 kwa mujibu sheria.



Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Idundilanga Martha Mgaya  amesema zoezi hilo litahusisha pia ukaguzi wa makazi ya watu achilia mbali maeneo ya kibiashara na Ofisi.


Nao wakazi wa mtaa wa Idundilanga  wamesema elimu ya umuhimu wa kutunza mazingira inahitajika kutolewa mara kwa mara kwa wananchi ili kudumisha utamaduni wa kufanya usafi.



Baada ya kuzinduliwa rasmi katika Mtaa huo kampeni hiyo inahamia Mtaa wa Sido Julai 2 mpaka itakapofikia tamati Julai 10 mwaka huu kwa kufanya usafi katika Soko kuu chini ya mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa.



Halmashauri ya mji wa Njombe inaendelea kuweka mazingira katika hali ya usafi na salama ikiwa ni mkakati wa mwendelezo wa kujinyakulia tuzo za usafi kwa kushika nafasi ya kwanza Kitaifa katika mashindano ya Usafi wa mazingira kwa miaka kadhaa mfululizo.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI