NA JOSEA SINKALA, SONGWE.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA jimbo la Vwawa wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, kimesema kitahakikisha kinashinda uchaguzi wa Serikali za mitaa vitongoji na vijiji pamoja na uchaguzi mkuu wa mwakani ili kulikomboa Taifa (Tanzania).
Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la Vwawa Mchungaji Amoni Mwashitete angali akizungumza na wananchi wa kata ya Hasamba jimbo la Vwawa wilayani Mbozi kwenye mwendelezo wa ziara yake ya mikutano ya hadhara katika kata na vijiji mbalimbali jimboni humo.
Mwashitete ambaye pia ni mtia nia wa ubunge jimbo la Vwawa mwaka 2025 (CHADEMA), amesema CHADEMA imejipanga kuongoza nchi kuanzia Serikali za mitaa hivyo kuwaomba wananchi kuichagua CHADEMA wakati utakapowadia na kuhimiza kwenda kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye daftari la wapiga kura.
Kiongozi huyo wa upinzani anasema Chama Cha Mapinduzi kimeongoza nchi bila mafanikio halisi kwa zaidi ya miaka sitini hivyo Chama hicho kimekataliwa na Mungu mbinguni na badala yake CHADEMA ndio italeta mabadiliko ya kweli.
Mchungaji Mwashitete amewatuhumu viongozi wa Serikali za vitongoji tisa vinavyounda kata ya Hasamba kuwa wameuza mlima Hasamba, hawasomi mapato na matumizi, kushamiri kwa kodi na tozo lukuki kwenye maeneo mbalimbali pamoja na kutosimamiwa ipasavyo kwa raslimali za Taifa.
Kwa upande wake katibu wa Chama hicho jimbo la Vwawa Kalyembe Mshani, amesema Serikali imesababisha chuki baina ya wananchi na viongozi wao hasa viongozi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji kwa kupita bila kupingwa vitendo anavyosema hawataruhusu kwenye chaguzi zijazo.
Pamoja na mengineyo kadhaa, katibu Mshani amesema Serikali imepandisha bei ya huduma ya umeme ambao sasa umekuwa kero kwa wananchi.
Naye katibu mwenezi wa CHADEMA jimbo la Vwawa Seleman Mgalla, amewaeleza wananchi kuwa wanapaswa kuichagua CHADEMA kwasababu sasa Serikali imechangia kwa asilimia kubwa wananchi kuwa na maisha magumu, bidhaa mbalimbali kupanda bei hivyo kuwataka wasimamizi wa chaguzi zijazo kutenda haki badala ya kuruhusu mfumo wa kupita bila kupingwa hatua anayosema haitavumiliwa.
0 Comments