NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Halmashauri ya wilaya ya Mbeya imepokea fedha zaidi ya shilingi million 250 kwa kipindi cha miezi sita ya Januari - Juni 2024 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akitoa taarifa ya utekelezaji miradi mbalimbali kwa Halmashauri ya Mbeya, afisa kutoka idara ya mipango Halmashauri hiyo Ozana Omary, kwaniaba ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri, amesema walipokea fedha zaidi ya shilingi million 264 ambazo katika kipindi hicho zimefanya kazi mbalimbali ikiwemo kwenye idara za elimu, afya, barabara, maji na ujenzi wa miundombinu lukuki.
Akizungumza kwenye mkutano huo wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbeya vijijini, Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza ameishukuru Serikali kuu kwa kutoa fedha zisizopungua Billion mia tatu kwa ajili ya Mbeya vijijini na kuwashukuru viongozi hao kwa maombi yao kwake kuona Mbeya vijijini inabadilika.
Pamoja na miradi mingine lukuki, Mbunge huyo amesema kuanzia baadaye mwezi ujao (Agosti 2024) mpango wa ujenzi wa barabara ya Mbalizi Shigamba utaanza kutekelezwa na kwa kuanza tayari fedha shilingi Billion mbili zimekwishatolewa ili kuanza utekelezaji mradi huo.
Njeza amewaomba viongozi katika maeneo yao kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na ofisi yake.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbeya vijijini Akimu Sebastian Mwalupindi amewapongeza viongozi mbalimbali kwa ushirikiano pamoja na wataalam kushirikiana na madiwani na ofisi ya Mbunge kufanya kazi huku akimtaka Mbunge na madiwani kuandaa mikutano ili kwenda kueleza kazi zinazofanywa na Serikali kama ilivyoahidiwa na chama chake.
Aidha kiongozi huyo amewataka wataalam kuendelea kufanya kazi kwa bidii na maarifa na kumwagiza mkuu wa wilaya hiyo kuhakikisha ndani ya siku kumi na nne anawasilisha majibu ofisini kwake (CCM Wilaya) juu ya majibu ya hoja na maswali yaliyoulizwa na wajumbe wa mkutano huo.
Katibu tawala wilaya ya Mbeya Azizi Mohamed Faki kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Mbeya Mhe. Benno Malisa, amesema Serikali kupitia watumishi wake itaendelea kusimamia nidhamu na weledi katika kufanya kazi kama ilivyoagizwa na chama tawala CCM.
0 Comments