NA JOSEA SINKALA, MOMBA SONGWE.
Naibu waziri wa madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, ameuagiza uongozi wa kijiji cha Ntungwa kata ya Mkomba Momba mkoani Songwe kwa kushirikiana na Halmashauri ya Momba na tume ya madini kuwasaka watu wawili wanaodaiwa kuingia kinyemela katika msitu wa kijiji hicho na kuanza shughuli ya madini ya Ulanga bila taarifa wala vibali vyovyote kutoka Serikalini.
Inaelezwa kuwa madini hayo yameanza kuchenjuliwa kutoka kwenye masalia ya msituni humo ambayo yapo tangu kipindi cha ukoloni ambapo raia hao mmoja wa kigeni na mwingine mzawa inadaiwa kuwa walienda kuripoti kwa uongozi wa kijiji na kutakiwa kutafuta vibali Halmashauri ili kuendesha shughuli hizo lakini hawakurudi kwa taarifa yoyote hadi Julai 04, 2024 walipobainika kuendesha shughuli hizo.
Hayo ni kwa mujibu wa Afisa mtendaji wa kijiji cha Ntungwa Ipyana Mwansasu alipoeleza mbele ya naibu waziri wa madini alipotembelea eneo la madini hayo akiwa ziarani wilayani Momba kwa mwaliko wa Mbunge wa Momba.
Mbunge wa jimbo la Momba Mhe. Condester Sichalwe (Namundi) ameeleza kusikitishwa na taarifa hizo ambazo zinalenga kuikosesha mapato Serikali na wananchi kwa ujumla kwa watu hao wasiofahamika kuanza kuchakata madini bila vibali.
Kufuatia hayo na ziara yake mahali hapo ambapo hakukutwa mtu yeyote, Naibu waziri wa madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, ameelekeza uongozi wa kijiji na ngazi za juu katika Halmashauri ya Momba kuweka ulinzi eneo hilo na kuwatafuta watu wanaodaiwa kuanza kufanya shughuli za madini hayo ya Ulanga bila kibali na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
0 Comments