Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA) imetangaza kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Kijiji cha Kalalangabo Kigoma Vijijini kutokana na kukamilika kwa upanuzi wa mradi wa maji kwenda kwenye kijiji hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Poas Kilangi akizungumza wakati kamati ya maendeleo ya kata ya ziwani Halmashauri ya wilaya Kigoma ilipofanya ziara kutembelea mradi huo alisema kuwa mradi huo unatarajia kukamilika Julai 15 mwaka huu na huduma ya maji kuanza kupatikana kwa wananchi.
Kilangi alisema kuwa mradi huo unatarajia kugharimu kiasi cha shilingi milioni 169 na hadi sasa mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 80.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa KUWASA alisema kuwa hatua ya kuboresha chanzo hicho cha maji inatokana na malalamiko ya wananchi wa kijiji cha Kalalangabo kukosa huduma ya maji kwa muda mrefu hali ambayo imekuwa na athari kubwa kwa Maisha yao ya kila siku ambapo awali Mkurugenzi huyo aliahidi kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.
Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Kijiji cha Kalalangabo, Shamsi Ismael amesema kuwa kwa kipindi kirefu wananchi wa kijiji hicho wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji hivyo kulazimika kutumia maji yasiyo safi na salama ikiwemo maji ya ziwa ambayo hayatatiwa dawa.
Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Kalalangabo, Lawina Chamlanga amesema kwa kipindi kirefu wananchi wa kijiji hicho hasa wanawake na watoto wamekuwa wakiteseka kwa kutafuta huduma ya maji hivyo kusababisha migogoro katika ngazi ya familia na kurudisha nyuma maendeleo ya Wananchi, Jamii na Taifa kwa ujumla.
Mwananchi huyo amepongeza kwa upanuzi wa mradi huo ambao unaenda kuwa mkombozi kwao katika kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama ambapo wameipongeza Mamala ya Maji Safi na Usafi Mazingira (KUWASA) kwa kusikiliza kilio cha wananchi wa kijiji hicho na kutekeleza mradi huo ambao unatatua kero ya upatikanaji maji kwa wananchi.
Mwisho.
0 Comments