
MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NCHINI JAJI FRANCIS MUTUNGI
Na Fatma Ally, Matukio DaimaApp, Dar
Msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Francis Mutungi amevitaka vyama vya siasa kuepukana na migogoro ya kisiasa kwani inapasua vyama na taifa kwa ujumla, huku akitaka vyama hivyo kuendeshwa kitaasisi.
Rai hiyo ameitoa leo jijini Dar es Salaam leo wakati alipokua akifungua mafunzo ya siku mbili kwa viongozi wa vyama vya siasa nchini ikiwa mafunzo ya maandalizi ya bajeti ya chama cha siasa, lengo ni kujenga mabadiliko ya uendeshaji wa vyama hivyo .
Aidha, Jaji Mutungi amevitaka vyama hivyo kuyatumia mafunzo hayo kama chachu ya mabadiliko ndani ya chama katika uendeshaji huku akiwataka viongozi wake kujiepusha kuhamasisha vitu ambavyo vinavuruga nchi, wafuasi wengi watawafuata ikiwa watafanya mambo mema.
Amesema kuwa, vyama vya siasa ni Taasisi ya umma hivyo vinapaswa kusajiliwa na kutenda majukumu yanayotambulika kidemokrasia na kuachana na vurugu ambazo zinasababisha vyama hivyo kuwa na mpasuko na.
"Haya mafunzo yataendelea, tuyatumie kwa umakini mkubwa kwani pesa hizi ni kodi ya wananchi, hivyo yatasaidia kuepukana na mambo mbalimbali ikiwemo mogogoro ya ubadhirifu wa fedha ndani ya chama na kuingia kwenye matumizi mabaya, hali ambayo imekua ikiripotiwa kwenye taarifa ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali CAG"amesema Jaji Mutungi.
Aidha, amevitaka vyama vya siasa kuwa vinara wa kujenga nchi na kwamba Tanzania sio nchi ambayo inapata utawala kwa mabavu bali ni demokrasia iliotukuka.
KATIBU WA ACT - WAZALENDO ADO SHAIBU
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa ACT - Wazalendo Ado Shaibu amesema kuwa migogoro ya vyama vya siasa inapaswa kutatuliwa kwa njia ya maridhiano, hivyo watayatumia mafunzo hayo na rai iliyotolewa na msajili katika kujiimarisha vizuri kisiasa ndani ya chama chao.
"Ni kweli migogoro inapasua vyama, inaleta mvurugano mkubwa hasa baada ya uchaguzi, tutakua tukimaliza migogoro yetu ndani ya chama wenyewe kwa njia ya maridhiano, tunaishukuru ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kutuletea mafunzo haya ambayo yatasaidia kuondoka migogoro kwenye vyama vyetu"amesema Ado.
Naye, Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Demokratic Part (DP) Philipo Fumbo amesema vyama vya upinzani (vidogo) vimekua vikikabiliwa na changamoto ya ruzuku jambo ambalo linapelekea kushindwa kuajiri wahasibu, lakini kupitia mafunzo hayo wataweza kuendesha vyama vyao na kuepuka matumizi mabaya ya fedha za vyama.
Aidha, ameshukuru ofisi ya msajili kuwapatiwa mafunzo hayo ambapo watayatumia kwa umakini mkubwa na kumaliza tofauti zao ndani ya chama kama msajili alivyoagiza ili kuepusha migogoro na mpasuko ndani ya chama .
0 Comments