Header Ads Widget

HOJA ZA CAG KAA LA MOTO KWA HALMASHAURI KIGOMA

 


Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 

HALMASHAURI za mkoa  Kigoma zimetakiwa  kuzifanyia kazi na kuzifunga  hoja zote za Mdhibiti na Mkaguzi wa serikali zilizoibuliwa kwenye halmashauri zao na kwamba kufikia Julai 30 mwaka huu hoja hizo ziwe zimefungwa.

 

MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye ametoa maagizo hayo akizungumza na madiwani na wakuu wa idara za halmashauri ya wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma wakati wa baraza maalum la kuwasilishwa kwa hoja za CAG za mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo ametoa siku 30 agizo hilo liwe limetekelezwa.

 


Katika mkutano huo Mkuu huyo wa mkoa aliagiza halmashauri zote za mkoa Kigoma  hadi kufikia Julai 30 ziwe zimefunga hoja hizo na maagizo la LAAC huku wilaya ya Uvinza ikiwa na hoja 29  za mwaka wa fedha 2021/2022 na hoja 24 za mwaka wa fedha 2022/2023.

 

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa kufanya kwa kwa mazoea kwa watalaam bila  sheria,kanuni na taratibu bila  kutumia taaluma zao katika kushughulikia  masuala ya fedha na usimamizi wa majukumu yaliyo chini yao ndiyo sababu kubwa ya kuibuka kwa hoja hizo.

 


Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkuu wa ofisi ya Mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali mkoa Kigoma, Nelson Rwezaura alisema kuwa sababu kubwa ya kuzaliwa kwa hoja kunatokana na idara zote kutofanya kazi kwa ushirikiano na watendaji wengi wanadhani ukaguzi huo unahusu idara ya fedha bila kutilia maanani kwamba idara zinazofanya matumizi zinawajibu wa kufuata sheria na taratibu za fedha.

 

 

Akiwasilisha hoja hizo za CAG kwenye kikao hicho cha baraza Mkaguzi wa ndani wa halmashauri ya wilaya Uvinza, Benedict Kiranda alisema kuwa jumla ya hoja 24 zimeibuliwa kwenye  mwaka wa fedha 2022/2023 huku sehemu kubwa ya hoja hizo zikianguka katika mapungufu ya nyaraka na maelezo yasiyojitosheleza ya matumizi ya fedha na utekelezaji wa shughuli zilizopangwa.

 


Akifunga kikao hicho cha baraza Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Uvinza, Jackson Mateso alisema kuwa wamepokea maelekezo na maagizo yaliyotolewa na kwamba watayafanyia kazi kuhakikisha hoja zinafungwa lakini wanaweka mikakati ya kuhakikisha halmashauri haizalishi hoja mpya.

 

Mateso alisema kuwa katika hilo halmashauri hiyo ambayo imepata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo na kufanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji mapato itasimamia sheria,kanuni na taratibu zinazoongoza utendaji wa halmashauri ili kuwezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa wananchi bila kuwepo ukiukwaji wa taratibu za fedha na utendaji.

 

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI