Header Ads Widget

BASI LAGONGA DARAJA, LATUMBUKIA MTONI, WAWILI WAPOTEZA MAISHA.

Na Moses Ng'wat, Mbozi.

WATU wawili wamefariki  na wengine 16 kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria  kugonga nguzo ya daraja na kutumbukia mtoni.

Akithibitisha kutokea kwa ajili hiyo ambayo imetokea leo Julai 15, 2024, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Gallus Hyera  amesema basi hilo la Ngasere High Class lenye namba T  547 ECX lilikuwa likitokea Dodoma kuelekea katika mji wa mpakani wa Tunduma Mkoani Songwe.

Amesema kuwa basi hilo baada ya kufika eneo la mteremko mkali katika kijiji cha Myovizi, Wilayani Mbozi lilimshinda dereva na kwenda kugonga nguzo ya daraja kisha kutumbukia mtoni na kusababisha vifo hivyo na majeruhi.

Kaimu Kamanda Hyera  ameongeza kuwa,  katika ajali hiyo watu wawili walifariki papo hapo na wengine 16 walijeruhiwa na kukimbizwa Hospitali ambapo walipatiwa matibabu na kuruhusiwa huku majeruhi wawili wamebaki hospitalini hapo wakiendelea na matibabu kutokana na hali zao kuwa mbaya.

Kaimu Kamanda Hyera,  amewataja waliofariki kuwa ni Henry Msakila (29) na Ipyana  Mwaibambe (47) wote wakazi wa Mkoa wa Dodoma.

Aidha, Kaimu Kamanda Hyera amewataja majeruhi wawili ambao bado wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya serikali ya Vwawa iliyopo Wilayani Mbozi kuwa ni Dereva wa basi hilo Salim  Mlelwa (42) Mkazi wa  Iringa ambaye amevunjika ubavu mmoja  pamoja na kondakta wake Zainabu Bakari (19) Mkazi wa  Kondoa mkoani Dodoma.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI