Header Ads Widget

ACT WAZALENDO WADAI KUWA ZANZIBAR INAHITAJI MAMLAKA KAMILI





Mwenyekiti wa Taifa wa  ACT-Wazalendo, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema ni ndoto kuleta maendeleo katika sekta yoyote Zanzibar kama haitakuwa na mamlaka kamili.


Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameyasema hayo leo Jumamosi, Julai 28, 2024 wakati alipokuwa akiwahutubia viongozi, wanachama, wapenzi na wafuasi wa Chama chake, akiwa Mgeni Rasmi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika Uwanja wa Kipangani jimbo la Ole, Mkoa wa Kusini Pemba.


"Mamlaka ndio nchi na ndio uchumi, maana hata mkopo huwezi kupata kama huna mamlaka, na cha kustaajabisha ni kuona wanaojiita watawala hawana hata wivu wa maendeleo na uchungu wa nchi yao", amesisitiza Othman


Aidha amesema umoja, mshikamano na usawa unaotakiwa kwa watu ndiyo chachu ya kuleta mabadiliko na maendeleo, hivyo ipo haja ya msingi ya kuungana na kuitetea nchi ili kuijenga Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja na yenye Mamlaka Kamili.


Akihutubia hadhara hiyo Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Zanzibar), Ndugu Ismail Jussa, amesema, ili kumuenzi Maalim Seif jambo kubwa ni kumuweka mrithi wake Mheshimiwa Othman mahala sahihi na si pengine bali ni Ikulu ya Zanzibar ili asimamie misingi ya kuirejeshea Zanzibar hadhi yake.


Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo, Mansoor Yussuf Himid, amesema ukweli, udhati na nia njema ya Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, ndio kilichomvutia kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga naye kwa lengo na dhamira ya kuitafuta Zanzibar yenye mamlaka kamili.


"Ili kukwamuka hapa ni lazima tuukwamue uchumi wetu na kuwajengea wananchi maisha bora, na njia pekee ni kuisambaratisha CCM na kuiweka ACT Wazalendo madarakani", amesisitiza Mansoor.


Alisema CCM haina uhalali wa kujinasibisha na Chama cha Afro Shirazi na Muasisi wa Mapinduzi, Sheikh Abeid Amani Karume kwa sababu hawasimamii chochote katika misingi iliyowekwa na ASP na Mzee Karume. "Ni tusi kwa CCM kujinasibisha na ASP", alisema.


Mapema, akifungua mkutano huo, Katibu wa ACT Wazalendo wa Mkoa wa Chake Chake kichama, Ndugu Saleh Nassor Juma, amesema Mkoa wa Chake Chake kichama upo imara na wanasubiri Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 ili kumpeleka Mheshimiwa Othman Masoud Ikulu akiwa Rais wa Zanzibar. 


Viongozi wa ngazi mbali mbali wa Chama hicho wakiwemo Wajumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu, Wabunge na Wawakikishi wamehudhuria Mkutano huo wakiongozwa na Katibu wa Oganaizesheni na Wanachama, Ndugu Omar Ali  Shehe.


Kabla ya mkutano huo, Mheshimiwa Othman alipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na wazee wa Mkoa wa Kichama wa Wete, ikiwa ni sehemu ya kusikiliza changamoto zao. Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Skuli ya Idrissa Abdulwakil, Kizimbani, Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.


Mheshimiwa Othman yupo kisiwani Pemba kwa ziara ya siku tano (5) inayojumuisha shughuli za Kisiasa, Serikali na kijamii, akiwa ameambatana na mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib.













Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI