Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA
CHAMA cha ACT Wazalendo kimesema tatizo la vijana kuzunguka na bahasha zenye vyeti hadi zinachakaa kwa ajili ya kusaka ajira litaondoka hapa nchini iwapo tu serikali itaongeza nguvu zaidi katika kuwekeza kwenye kilimo na sekta binafsi ambako ndiko kunapatikana ajira nyingi.
Kiongozi wa chama hicho, Doroth Semu, alisema hayo jana wakati akiwahutubia wananchi wa Manispaa ya Singida iliwa ni siku yake ya pili ya ziara mkoani Singida kuhamasisha wananchi wakiunge mkono ili kufikia lengo la kuandikisha watu milioni 10 ndani ya miezi 10 ambalo kimejiwekea.
"Wote tunajua asilimia 61 ya ajira za Watanzania ipo kwenye kilimo tulitegemea angalau serikali ingeona hapa ndio mahala bora pa kuwekeza na kuweza kupata matunda haraka ya watu kuajiriwa,leo hii kilimo chetu kinagubikwa na changamoto kibao bei zenyewe za mazao hazieleweki," alisema.
Semu alisema pamoja na kwamba asilimia 25 ya kipato chetu kinatokana na likimo lakini katika hali ya kushangaza kile kinachorudishwa ni kidogo sana na hii inatoa picha namna ambavyo serikali haijawekeza vya kutosha katika kilimo.
"Tunashindwa kukitumia kilimo kama eneo la kubadilisha maisha watanzania ambao asilimia 61 wanategemea kilimo, huku kwenye kilimo hatuoni maafisa ugani,pembejeo hazitoshi,hivi karibuni kulikuwa na changamoto ya mbolea ya ruzuku ambayo ndo tu kwanza imeisha karibuni," alisema.
Aliongeza kuwa serikali ya CCM imeshindwa kuwekeza kwenye nguvu kazi tuliyokuwa nayo kwani asilimia 58 ya watanzania wenye umri kati ya miaka 15 hadi 65 wako kwenye umri wenye nguvu ya kufanyakazi lakini hatuoni mazingira wezeshi ili watu waweze kufanya kazi zitakazowapatia kipato.
"Singida nyie mnalima alizeti leo hii bei ya alizeti haieleweki inabadilika leo hivi kesho vile,wapo watu wa katikati wa kutosha alimradi mkulima anazidi kuwa mnyonge badala ya mkulima kuneemeka badala yake wale watu wa katikati wananufaika na kilimo,"alisema.
Semu alisema kwa kutambua tatizo la ajira lililopo nchini,ACT Wazalendo katika sera zake kinawekeza kwenye kwenye kilimo ili kupata ajira nyingi ambazo zitazalisha kazi kwa ajili ya kuwasaidia vijana.
"ACT itaweka sera kuondoa vikwazo kusaidia mtu yeyote anayetaka kuanzisha kiwanda au kuanzisha shughuli ya kupata kipato ili shughuli zisizokuwa na tija ziondoke,"alisema.
Naye Naibu Mwenezi wa ACT Wazalendo Taifa, Shangwe Ayo,aliwataka wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura halafu siku ya uchaguzi wawachague wagombea kutoka chama hicho ili waweze kuona mabadiliko.
Shangwe alisema katika hospitali ya mkoa wa Singida wananchi wanalalamikia huduma mbovu za afya na kwamba hospital hiyo haina wahudumu wa afya wa kutosha.
Naibu Mwenezi huyo aliwasisitiza wana Singida kuichagua ACT Wazalendo kwani chama chenye sera bora ya hifadhi ya jamii kwa wote itayo wapa bima watanzania wote na kutibiwa bila kujali tatizo ni kubwa kiasi gani.
MWISHO
0 Comments