Header Ads Widget

WACHIMBAJI MADINI SONGWE WAMLILIA RAIS SAMIA AWAOKOE



Na Thobias Mwanakatwe 


WACHIMBAJI  wadogo wa madini wapatao 300 katika kijiji cha Kampilipili kilichopo kata ya Mbangala Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mgogoro uliopo katika machimbo hayo ambao umesababisha waondolewe eneo hilo. 


Walisema tangu mwaka 2011 wamekuwa wakichimba madini katika eneo hilo kwa ajili ya kujipatia pesa ya kuendeshea maisha na familia zao bila usumbufu wowote na serikali ilikuwa inafahamu uwepo wao katika eneo hilo tangu kipindi hicho na walikuwa wanalipa mapato kwa serikali.



Mwenyekiti wa wachimbaji hao, Goodluck Mungure,alisema katika hali ya kushangaza hivi karibuni wataalam kutoka ofisi ya madini wakiongozwa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Songwe, Chone Malembo walienda kutambulishwa ujio wa mwekezaji katika eneo hilo.


Alisema jambo hilo limewashangaza kwani kwa takribani miaka 13 wamekuwepo eneo hilo wakichimba madini na kufauta taratibu na sheria kama serikali inavyotaka lakini wameshangaa kuelezwa eneo hilo amepewa mwekezaji ambaye hata hivyo hawajawahi kumuona na wala hajawahi kufika katika kijiji hicho.



Wachimbaji hao walisema kitendo cha kuwaambia waondoke eneo hilo kwa kuwa tayari limepewa mwekezaji kimewashtua kwa kuwa tangu mwanzo hawakuwahi kushirikishwa tangu mwanzo wa mchakato huo  lakini ghafla anakuja kuletwa mwekezaji jambo ambalo ni kuwakandamiza wachimbaji wadogo.


Waliongeza kuwa kimsingi wao hawapingani na serikali katika suala la kutafuta mwekezaji katika eneo hilo lakini kabla ya kufanya hivyo wangeshirikishwa wachimbaji wadogo wa madini ambao wamekuwepo eneo hilo kwa muda mrefu badala ya kuwashtukiza waondoke wakati tayari na wao walikuwa wamewekeza fedha zao katika kuchimba madini kulingana na uwezo wao.



Walisema kuondolewa ghafla eneo hilo bila kutafutiwa njia mbadala maana yake ni kuwaangamiza wachimbaji wadogo kiuchumi wakati serikali inatambua wachimbaji wadogo wa madini ambao nao ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi kupitia sekta ya madini.


Walisema suala hili kuna jambo limejificha nyuma ya pazia ambapo inawezekana kuwa watu wapo nyuma ya jambo hili kwa ajili ya kulinda maslahi yao binafsi.



"Tumekopa fedha katika taasisi za fedha kwa ajili kununua vifaa vya uchimbaji vijavyolingana na uwezo wetu sasa leo hii tunapoambiwa tuondoke ili apewe mwekezaji mwenye fedha zake huu ni unyanyasaji wakati na sisi ni watanzania na tuna haki ya kufaidi matunda ya raslimali za nchi hii," walisema wachimbaji hao.


Waliongeza kuwa kinachowapa mashaka ni kwamba Afisa Madini  Mkoa Songwe aliyeanza mchakato wa kutoa leseni kwa mwekezaji ni Laurent Mayala ambaye kwa sasa amehamishiwa Mkoa wa Mbeya.



Naye Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo Mooa wa Songwe, Bw.Kamaka alisema haiwezekani mwekezaji apewe eneo hilo la wachimbaji ambao wamekuwepo kwa muda mrefu ambaye kwanza hajulikani.


Anasema serikali iingilie kati haraka suala hili kunusuru kuvunjika kwa amani eneo hilo hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa.


Afisa Madini Mkoa wa Songwe,Chone Malembo, alipoulizwa alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na kwamba umeanza baada ya kwenda kumtambulisha muwekezaji katika eneo hilo.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomoni Itunda  ametoa agizo kusimamisha shughuli zote za uzalishaji katika eneo hilo kwa sababu za kiusalama.


"Nakuagiza Afisa Madini Mkoa shughulikia suala hili kwa kushirikisha pande zote ili kuoata suluhu," alisema.


MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI