UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) Kibaha Mjini umelaani tukio la kuuwawa mtoto mwenye Ualbino Asimwe Novath (2) huko Muleba Mkoani Kagera.
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza kuu la umoja huo lililofanyika mjini Kibaha Mwenyekiti wa Uwt Kibaha Mjini Eline Mgonja amesema tukio hilo la kukatisha uhai wa mtu mwingine halikubaliki.
Mgonja amesema kuwa wanalaani kwa nguvu zote kitendo cha mauaji ya mtoto huyo ambaye hana hatia na vitendo hivyo vya ukatili havikubaliki ndani ya jamii.
"Watu waachane na dhana potofu kuwa wakipata viungo vya albino vitawasaidia katika kupata mali au kwenye masuala ya uongozi watu hao wananyima haki za wengine hivyo hatua kali zichukuliwe,"amesema Mgonja.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka kwa kuisaidia huduma ya maji na jiko la gesi familia yenye watoto wawili wenye ualbino.
Nyamka amesema kuwa Koka aliwapelekea huduma ya maji kwani eneo hilo maji yalikuwa yakipatikana mbali hivyo kukawa na hatari watoto hao kuweza kufanyiwa vitendo vya ukatili wakati mama akiwa anaenda kutafuta maji.
Amesema kuwa baada ya kufanikisha hilo alikabidhi jiko kwa familia hiyo ili isihangaike kwenda kutafuta kuni mbali na kuwaacha watoto hao peke yao hivyo watoto hao kuwa hatarini.
Mwisho.
0 Comments