Header Ads Widget

RAIS SAMIA AFANYA MAGEUZI MIUNDOMBINU YA BARABARA SAME.

 



DC AMSHUKURU BAJETI YA TARURA YAPAA KUTOKA MILIONI 660 HADI BILIONI 6.7 KWA MWAKA. 


NA WILLIUM PAUL, SAME. 



BAADHI ya wakazi wa Kata ya Makanya Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 410 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Makanya kwa teknolojia ya mawe urefu wa Mita 46 ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 95%.



Ujenzi wa daraja hilo linalo unganisha Kata ya Makanya na Suji sehemu ya uboreshaji wa Miundombinu ya barabara ya Makanya - Suji - Mweteni yenye urefu wa kilomita 25 ambayo baadhi ya maeneo yake yaliathiriwa na mvua kubwa za masika zilizonyesha na kupelekea mawasiliano ya Kata za tambarare na milimani kukatika. 
 

Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni akiwa kwenye muendelezo wa ziara zake za ukaguzi wa miradi ya maendeleo alifika kwenye daraja hilo kujionea hali halisi ya utekelezaji wake ambapo amemuagiza Meneja wa Wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA Mhandisi Mnene James kuhakikisha kazi zilizosalia kukamilisha ujenzi wa daraja zinafanyika haraka iwezekanavyo ili wananchi waweze kunufaika na fedha zilizotolewa na Rais.



Aidha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwapatia fedha kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara, lakini pia amempongeza Meneja wa TARURA Wilaya hiyo Mhandisi Mnene James kwa usimamizi mzuri kwa Mkandarasi kuhakikisha daraja linajengwa kwa viwango vinavyostahili kwa mujibu wa mkataba unavyomtaka.


“Kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia madarakani bajeti ya TARURA Wilaya ya Same imeongezeka mara dufu zaidi kutoka shilingi milioni 660 kwa mwaka hadi kufikia zaidi ya bilioni 6.7 hii imesaidia sana wananchi kufika sehemu ambazo zilikuwa hazifikiki”. Alisema DC Kasilda.



Kwaupande wake Mhandisi Mnene amesema matumizi ya teknolojia ya mawe kwenye ujenzi wa madaraja inasaidia kupunguza gharama za ujenzi ikilinganishwa na matumizi ya zege ambapo daraja hilo lingejengwa kwa zege lingetumia zaidi ya shilingi biloni 2.2 lakini kwa teknolojia ya mawe limejengwa kwa zaidi ya shilingi milioni 399.


Alisema kuwa, TARURA wataendelea kuitumia teknolojia hiyo kwenye miradi yote ya barabara wanayotarajia kuijenga hivi karibuni katika mwaka wa fedha 2024/25.


Mwisho. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI