Header Ads Widget

POLISI SONGWE YAWATAKA WAUMINI KUSHIRIKIANA NAO KUKOMESHA UKATILI, UHALIFU.

NA JOSEA SINKALA, SONGWE.

Jeshi la Polisi Mkoani Songwe limewaomba waumini wa Kikristo na wananchi kwa ujumla katika Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe, kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo ili jamii ichukie uhalifu na wahalifu ikiwa ni pamoja na vitendo viovu vinavyofanyika katika maeneo yao.


Kauli hiyo imetolewa na kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga wakati akizungumza na waumini wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) lililopo Kata ya Mlowo Wilayani Mbozi chini ya Mchungaji kiongozi wa kanisa hilo John Mwaisabila pamoja na wananchi wengine waliojumuika kwenye ibada ya mazishi ya kuaga mwili wa mmoja wa waumini wa kanisa hilo aliyefariki hivi karibuni.


Kamanda Senga, amewataka waumini kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kutokomeza vitendo vya uhalifu na ukatili wa kijinsia katika jamii.

Aidha, Kamanda Senga amewataka waumini hao kuendelea kueneza injili kwa jamii ili jamii iache matukio ya ukatili wa kijinsia pia kuepukana na tabia za kujichukulia sheria mkononi bali wafanye ukamataji salama kwa hatua zaidi ya kisheria.


Mkoa wa Songwe bado unakabiliwa na matukio ya ukatili, uhalifu na baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi mambo ambayo hayatakiwi kuendelea kushamiri katika jamii kwani kuishi ni haki ya kila mtu akifuata kanuni, taratibu na sheria za nchi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI