Naibu Waziri wa TAMISEMI Zainabu Katimba (wa pili kulia) akitembelea na kukagua barabara za manispaa ya Kigoma Ujiji zilizotekelezwa mwaka wa fedha 2023/2024 kupitia TARURA anayetoa maelezo ni meneja wa TARURA wilaya ya Kigoma Ellias Mutapima (katikati)
Naibu Waziri wa TAMISEMI Zainabu Katimba (wa pili kulia) akimsikiliza maelezo ya John Meena Mhandisi Mshauri wa mradi wa TACTICS unaotekelezwa katika manispaa ya Kigoma Ujiji wakati Naibu Waziri alipotembelea mradi huo.
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
NAIBU Waziri Tawala za mikoa na serikali za mitaa Zainabu Katimba ametaka wakandarasi wanaochelewesha miradi mbalimbali inayotekelezwa mkoani Kigoma bila kuwa na sababu muhimu kuchukuliwa hatua kulingana na sheria na taratibu za mikataba yao.
Katimba alisema hayo alipofanya ziara ya kiserikali mkoani Kigoma kutembelea miradi ya barabara ukiwemo mradi wa kuendeleza na kuboresha Miundombinu ya Miji Nchini Tanzania ( TACTICS) Manispaa ya Kigoma/Ujiji unaotekelezwa kwa mkopo kutoka benki ya Dunia.
Naibu Waziri huyo wa TAMISEMI alisema kuwa hakubaliani na taarifa ya Mhandisi Mshauri wa mradi huo, John Meena inayoeleza kuwa mradi huo hadi sasa umetekelezwa kwa asilimia 17 wakati ulipaswa kuwa umefika asilimia 35 na kwamba sababu ya uwepo wa mvua nyingi hazina msingi kwa sababu kazi iliyokuwa ikianza haikuwa inaathiriwa na mvua kwa kiasi cha kusimamisha mradi.
Akiwa kwenye ziara hiyo Naibu Waziri huyo alieleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya barabara chini ya Wakala wa barabara mjini na vijijini mkoa Kigoma (TARURA) na kuitaka taasisi hiyo kuwa wakali kwa wakandarasi ambao hawatekelezi shughuli zao kwa mujibu wa miakataba yao.
Awali mhandisi Mshauri wa mradi huo, John Meena kutoka kampuni ya Saba Engineering alisema kuwa kwa sasa mradi huo upo asilimia 17 nyuma ya utekelezaji ikiwa unapaswa kuwa asilimia 35 na kwamba mvua nyingi zimesababisha mradi kuchelewa.
Katika ziara hiyo Kaimu Meneja wa TARURA mkoa Kigoma, Alias Mutapima alimtembeza Naibu Waziri wa TAMISEMI kwenye barabara mbalimbali zilizotekelezwa kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 ikiwemo barabara zilizojengwa kwa zege katika maeneo ya miinuko ili kukabiliana na uharibifu wa barabara hizo wakati wa Mvua nyingi na madaraja ya mawe.
Mkuu wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye (kushoto) akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa TAMISEMI Zainabu Katimba (kulia aliyekaa) kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali mkoani Kigoma ambapo serikali imepeleka kiasi cha shilingi trilioni 11.4 tangu mwaka 2021 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mkoani Kigoma.
0 Comments