MAMA mjasiriamali mkazi wa Kata ya Mindu katika Manispaa ya Morogoro Bi Salama Lusala, anayefanya biashara ya kupika na kuuza Vitumbua amewahimiza wanawake wa maeneo hayo kujiunga vikundi na kufanya shughuli za kujiingizia kipato, sambamba na kuomba mikopo katika maeneo sahihi yanayotambulika kisheria, badala ya mikopo inayoweza kutweza utu wao.
Bi Salama Lusala alisema hayo wakati akitoa ushuhuda wake kwa wanawake wa kata ya Mindu, ulioandaliwa na Jumuiya ya Wanawake (UWT) ya chama cha mapinduzi katika kata hiyo uliokwenda sambamba na Baraza la Jumuiya hiyo ngazi ya kata.

Akaeleza namna alivyofaidika na mkopo wa shilingi milioni 18 uliotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kikundi cha watu 30 wa kata hiyo, uliowawezesha kupata bajaji tatu ambazo zimeendelea kuwaingizia kipato.
"Kikubwa ni uaminifu,mnapochaguana kuunda kikundi muaminiane, Kila siku nakiuza Vitumbua natenga shilingi 2000 kwaajili ya marejesho, tumefanikiwa kumaliza mkopo na sasa tunasubiri wakianza Tena kutoa tuombe mkubwa zaidi, watu wasiseme mikopo haitoki au haisaidii, lakini wajiepushe na Ile ya kausha Damu na yenye masharti magumu yenye nia ya kuwafilisi na kuwadhalilisha"Alisema Bibi huyo muuza Vitumbua.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mgaza Kata ya Mindu Specioza Model akasema katika mtaa huo vikundi vinne vilipata mkopo kutoka Halmashauri ya Manispaa kwa viwango tofauti na kuwaasa wananchi wanaoomba mikopo na kukosa kujifunza kwa wengine na kuulizia sababu zinazochangia kukosa.
Katibu wa UWT Kata ya Mindu Bi Sharifa Dutilo, akawataka wanawake wa kata hiyo kupendana, kujaliana na kusaidiana katika kufanikisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo sambamba na kuwaunga mkono na kuwashawishi kugombea wanawake watakaoona Wana sifa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.
Licha ya kuwaasa pia kutokubali kurubuniwa kuchukua mikopo chechefu ya fedha kutoka kwa watu binafsi, vikundi na taasisi mbalimbali zenye mikopo ya haraka lakini yenye masharti magumu na zinazodhalilisha kupitia mitandaoni ama kuwafuata mitaani wanapoishi, akawahimiza kuunda vikundi na kutafuta fursa sahihi zinazojitokeza ikiwemo mikopo ya Halmashauri inayotokana na asilimia 10 zinazotengwa kwaajili ya makundi ya wanawake, vijana na makundi maalum.
Naye Mlezi wa kata hiyo na Diwani wa viti maalumu (CCM) Manispaa ya Morogoro Bi Latifa Ganzel aliwahimiza wanawake kuhamasishana kufanya uhakiki kwenye daftari la kudumu la wapiga kura pindi zoezi hilo likifika kwenye maeneo yao na kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Ganzel akasema suala la kugombea ni haki yao kikatiba pindi muda wa uchaguzi ukikaribia, hivyo wasisite kufanya hivyo na kwa wingi pindi wakati ukifika.
Akawataka wanawake kujiamini, kuacha woga na kufanya shughuli za maendeleo hata kwa kuanza na kidogo kwa ubora, badala ya kutaka mambo makubwa kwa haraka na kuishia kuchukua mikopo ya kausha Damu inayowakimbiza majumbani au kusababisha kudhalilishwa.
Mwisho.
0 Comments