NA WILLIUM PAUL, SAME.
MKUU wa wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni ameyatahadharisha baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOS) ambayo yatajihusisha na mapenzi ya jinsia moja (ushoga) yatapigwa marufuku na kusitishwa kuendelea kutoa huduma za kijamii wilayani humo.
Amesema kipindi cha mwaka 2023 yapo mashirika yaliyochukuliwa hatua baada ya kubaini kujihusisha na vitendo hivyo kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Kata ya Makanya na sasa ameanza kuona dalili kuwa hali hiyo imerejea tena hivyo amewaomba wananchi kuendelea kuwa na tahadhari pia kutoa taarifa hata kwa siri wanapoona shughuli hizo za kuhamasisha mapenzi ya jinsi moja zikiendelea kwenye kwenye maeneo yao.
“Naumizwa sana na ushoga kwa sababu unaathiri maisha ya mtanzania kwa ujumla wake lakini ushoga unaondoa nguvu kazi ya vijana kwa sababu vijana wetu wanakuwa hawana nguvu hawana mwelekeo na hili Taifa ili liweze kuendelea tuwe na uchumi mzuri lazima vijana wafanye kazi”. Alisema DC Kasilda.
Kulingana na taarifa zilizopo Polisi Kitengo cha dawati la jinsia Wilaya ya Same mwaka huu 2024 jumla ya kesi nane za ukatili wa kijinsia zimeripotiwa nne kati ya hizo watuhumiwa wake wamehukumiwa wanatumikia adhabu Gerezani hata hivyo bado wapo baadhi ya wazazi wanao tumia kesi hizo kama mtaji kulipana fedha pindi mtoto anapofanyiwa ukatili.
0 Comments