NA JOSEA SINKALA, NJOMBE.
Wanachama na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika mikoa ya Kanda ya Nyasa hususani kutoka Baraza la Vijana wa Chama hicho (BAVICHA) wamelazimika kusafiri hadi mkoani Njombe kwa ajili ya kuwajulia hali wanachama na viongozi wenzao walio gerezani.
Wanachama kadhaa wa CHADEMA Kanda ya Nyasa wanaendelea kusota mahabusu wakikabiliwa kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kesi zinazohusishwa na masuala ya siasa hasa kwenye chaguzi zilizopita.
George Sanga ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la vijana wa chama hicho mkoa wa Njombe ni miongoni mwa wanasiasa ambao wanakabiliwa na kesi mbalimbali na George anatuhumiwa kwa shauri la mauaji mnamo mwaka 2020 kuelekea uchaguzi mkuu wa kipindi hicho na tayari kesi hiyo ya tuhuma za mauaji inaendelea kusikilizwa katika Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa.
Katika kuwaunga mkono wanasiasa hao, wanachama na viongozi wa Baraza la vijana hasa katika mikoa ya Songwe, Mbeya na Njombe wameongoza mchango wa fedha na vitu mbalimbali ili kwenda kuwajulia hali wanachama wenzao George Sanga na wenzake huko mkoani Njombe.
Okoka Mbwilo ni kaimu Mwenyekiti wa BAVICHA mkoa wa Njombe amewashukuru vijana na wanachama wote ndani ya CHADEMA kwa kuamua kuungana kwenda gerezani ili kuwajulia hali wenzao.
Naye Neema Mbwilo ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la wanawake BAWACHA jimbo la Makambako, amewapongeza wana-Chadema wawili waliobuni wazo la kuchangisha mchango ili kwenda kuwatembelea wenzao katika gereza la Wilaya ya Njombe.
Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Momba Ayubu Sikagonamo amehimiza umoja zaidi na mshkamano ndani ya chama hicho ili kuendelea kushikamana na kujenga uimara zaidi akisema CHADEMA ni familia moja na inaendelea kupambana na hujuma za wapinzani wao na kupigania maslahi ya Taifa.
Sikagonamo amesema katiba mpya na tume huru ya uchaguzi ni baadhi ya mambo ambayo yanadaiwa na wananchi wa Tanzania ili kuleta nidhamu katika kuongoza badala ya kuonea watu na kuwaweka magereza bila makosa ya msingi ikiwemo mfumo wa kukamata watuhumiwa na kuwaweka kizuizini bila kuwa na upelelezi wa kuthibitika mambo ambayo anasema hayataruhusiwa kwenye katiba mpya.
Wanachama wa CHADEMA wanaendelea kujitoa kuchangia mambo mbalimbali kunapokuwa na uhitaji hususani misiba na matatizo mengine mbalimbali utaratibu unaoonekana kuwa kote nchini ndani ya chama hicho ikiwemo kupitia makundi ya mtandao wa WhatsApp.
0 Comments