Na Ashton Balaigwa,DODOMA
BENKI kuu ya Tanzania(BoT) imeonya watanzania wenye tabia ya kuharibu na kuifedheesha fedha ya Tanzania kwa kuiweka kwenye soksi,sehemu za siri,kuitengenezea mataji kwenye sherehe,kufunga kwenye kanga,matiti na kuweka chini ya magunia kuacha kufanya hivyo kwani ni kosa la jinai.
BoT imesema kuanzia sasa wale wote watakabainika watafikishwa kwenye vyombo vya kisheria ikiwemo Mahakamani kwakuwa fedha hizo ambazo ni Noti na Sarafu ni sehemu ya nyara za Serikali zinapaswa kuthaminiwa.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja Idara ya Uendeshaji wa Benki Kuu tawi la Dodoma Nalasco Maluli, wakati akiwasilisha mada kwenye mafunzo ya wandishi wa habari kutoka mikoa saba ya Tanzania bara.
Maluli alisema fedha hizo za Tanzania ni sehemu ya tunu ya taifa hivyo zinapaswa kuheshimiwa kama ilivyo Bendera ya Taifa na kuanzia sasa yoyote atakayebainika kuifedhesha atachukuliwa hatua za kisheria pasipo mashaka yoyote.
“ Nendeni mkawape elimu wananchi kuwa kuwa fedha ya Tanzania ni tunu ya Taifa hawatakiwi kuchana wala kuharibu kwani sheria imeshapitishwa tayari atakayebainika kuharibu tutamfikisha Mahakamani “ alisema Maluli.
Alisema fedha hizo za Tanzania zinatengenezwa kwa gharama kubwa kwa kutumia fedha za kigeni hivyo zinapotunzwa vizuri zitatumika kwa muda mrefu na kupunguza gharama ya kutengeneza fedha nyingine kwa kutumia fedha za kigeni.
Meneja Idara ya Uendeshaji wa Benki Kuu tawi la Dodoma,alisema wananchi wanapotunza fedha hizo itasaidia fedha za kigeni kutumika katika shughuli nyingine kama kwenye elimu,afya na miradi ya kimkakati pamoja na mambo mengine ambayo wananchi wanahitaji kufanyiwa na Serikali yao.
Naye Meneja Msaidizi Sarafu kutoka BoT tawi la Dodoma,Matilda Luunga,alisema umefika wakati kwa wafanyabiashara wa vitu mbalimbali kuacha kuweka fedha chini ya gunia kwani unyevunyevu unasababisha kuharibu fedha.
Alisema ipo tabia imejitokeza kwenye maharusi na sherehe mbalimbali wamekuwa wakitengeneza mataji ya fedha hizo kuacha tabia hiyo kwakuwa pesa haitengenezewi taji kwakuwa ni tunu ya taifa kama ilivyo bendera ya taifa.
Meneja Msaidizi Sarafu kutoka BoT alisema mwaka 2002 ulishatoka muongozo wa onyo wa kutodharau na kutofedheedha fedha ya Tanzania na mwaka 2001 kulishapitishwa sheria ya kuchukuliwa hatua kwa watakaobainika kufanya hivyo.
Meneja Idara ya Mawasiliano wa BoT Victoria Msina ,alisema wameamua kuwakutanisha waandishi hao wanatoka mikoa ya Iringa,Morogoro,Dodoma,
Alisema lengo lake kuwa daraja muhimu kati ya BoT na wananchi ili kuwafikia wananchi kwa karibu katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na Benki hiyo na kuleta matokeo chanya na kuleta maendeleo .
0 Comments