Wahadhiri wawili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) nchini Tanzania, wametua Nairobi, Nchini Kenya kutambulisha kitabu walichoandika kuhusu matarajio ya utangamano kwa kutumia mgogoro wa Sahara Magharibi kama moja ya changamoto kufikia utangamano wa bara la Afrika.
Wahadhiri hao Dk Maxmillia Chuhila na Dk James Zotto wamekitambulisha kitabu chao ambacho kimehaririwa na kuchapishwa na APE NETWORK katika hafla iliyofanyika Chuo Kikuu cha Kenyatta, jijini Nairobi nchini Kenya.
Hivi karibuni Zotto na Dk Chuhila walifanya uzinduzi wa kitabu hicho katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU), Mkoani Iringa nchini Tanzania.
Utambulisho wa kitabu hicho nchini Kenya unalenga kusambaza maudhui ya utangamano wa Afrika kwenye nchi za bara hilo huku kikichambua changamoto zinazo kwamisha Muungano wa Afrika.
Akizungumza katika wasilisho lake, Zotto amesema unahitajika ushirikiano wa pamoja wa Waafrika katika kufikia ndoto za utangamano licha ya kuwepo kwa tofauti za kikabila, lugha, tamaduni, Mila na desturi.
Kulingana na wanazuoni hao, umoja na
utangamano ni silaha laini ya kukabiliana na tishio lolote kutoka mataifa mengine.
Mawasilisho yao yameonesha kuwa eneo la Sahara limeona maendeleo ya kijamii na kiuchumi kutokana na juhudi zinazofanywa na serikali ya Morocco, na kuifanya kuwa kitovu cha maendeleo na uwekezaji.
Wanahistoria hao wawili walitoa wito kuwepo kwa mazungumzo madhubuti na yenye kujenga ili kukomesha mzozo huo wa muda mrefu kwa kuzingatia juhudi zilizofanywa na Umoja wa Mataifa na umoja wa Afrika kumaliza mzozo huu wa kihistoria.
Dk Chuhila ambaye ni Mwenyekiti wa Historia Tanzania amessisitiza kwamba suluhu ya mgogoro huo inatakiwa itoke ndani ya watu wa Morocco wenyewe na wale wa Sahara Magharibi.
0 Comments