Header Ads Widget

WAKIMBIZI WA BURUNDI KUKABILIWA NA HALI NGUMU, KUNYIMWA MISAADA

Mkurugenzi wa idara ya wakimbizi ya wizara ya mambo ya ndani ya Tanzania Sudi Mwakibasi (kulia) akitoa tamko kwa wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma (Picha na Fadhili Abdallah)

 

Na Fadhili Abdallah,Kigoma


SERIKALI imetangaza kwamba misaada ya kibinaadamu kwa wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa kwenye kambi za wakimbizi za Nyarugusu wilaya ya Kasulu na Nduta wilaya ya Kibondo itakoma ifikapo  Desemba 31 mwaka huu na wakimbizi hao watapoteza hadhi yao ya ukimbizi.

 

Mkurugenzi wa idara ya wakimbizi ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi, Sudi Mwakibasi akiongoza ujumbe wa watendaji wa idara hiyo alitangaza hilo kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma na katika mkutano wa hadhara na wakimbizi na kusema kuwa wakimbizi hao wanachopaswa sasa ni kurudi nchini mwao.

 

Mwakibasi alisema kuwa serikali ya Tanzania,Serikali ya Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) kwa niaba ya mashirika yanayotoa misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wamekubaliana kuwa ifikapo Desemba 31 mwaka huu kambi zote zinazohifadhi wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania zifungwe na wakimbizi wa nchi hiyo wanapaswa kuwa wamerudishwa nchini mwao.

 

Alisema kuwa kwa sasa mwelekeo wa dunia ni kusaidia wahanga wa mafuriko na maafa yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi na kwamba mashirika ya Umoja wa mataifa na washirika wake wamebadili mwelekeo wa kusaidia huduma za kibinadamu kwa wakimbizi ambao amani kwenye nchi zao imerejea na kuhamishia misaada hiyo kwenye maafa hayo.

Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa kambi ya Nyarugusi


Baadhi ya wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma akiwemo Masabo Alex alisema kuwa hawawezi kuondoka kambini humo kurudi Burundi kwa sasa kwani bado hali inayosemwa kuwa amani imerejea siyo ya kweli.

Mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) wilaya ya Kasulu Jean Bosco Ngomani 


Kwa upande wake Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) wilayani Kasulu mkoani Kigoma, Jean Bosco Ngomani alisema kuwa shirika lake kwa kusaidia na mashirika mengine yanayotoa huduma za kibinadamu kwa wakimbizi wataendelea kusaidia serikali ya tanzania kuhakikisha wakimbizi hao wa Burundi wanarudi kwao.

 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS