Na Fadhili Abdallah,Kigoma
SIKU chache baada ya serikali ya Tanzania kupitia wizara ya mifugo na uvuvi kuanza kutekeleza mpango wa kufunga shughuli za uvuvi katika ziwa tanganyika ikiwa ni makubaliano ya nchi nne zinazomiliki ziwa hilo, wadau wa uvuvi mkoani Kigoma wamesema kuwa hali imeanza kuwa mbaya na kuiomba serikali kutafakari uamuzi wake huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa Habari mjini Kigoma wadau hao wa uvuvi wakiwemo wamiliki wa boti za uvuvi na wavuvi walisema kuwa serikali inapaswa kufanya maamuzi mbadala kwani sehemu kubwa ya wananchi wanaotegemea rasilimali za uvuvi kuendesha Maisha yao wanaathirika kwa kiasi kikubwa.
Mmoja wa wadau hao , Frank Ruhasha alisema kuwa serikali ya Tanzania kupitia wizara ya mifugo na uvuvi inatekeleza jambo hilo ikiwa haina utafiti wa kina wa hatua hiyo na madhara yake huku hatua mbadala za kuanzisha vizimba vya kufuga Samaki ikiwa haina matokeo chanya kwani Samaki wameanza kufugwa baada ya ziwa kufungwa na hawataweza kuvuna wakati huu hadi ziwa litakapofunguliwa ambapo Samaki hao ndiyo watakuwa tayari kwa kuvunwa.
Kwa upande wake mmiliki wa boti za uvuvi katika mwalo wa Kibirizi manispaa ya Kigoma Ujiji, Moshi Haruna Rufunga alisema kuwa ana boti 12 za uvuvi ambazo zina wafanyakazi Zaidi ya 100 anakabiliwa na hali ngumu kwani watumishi wake hawakuwa na shughuli nyingine ya kufanya kabla kufungwa kwa ziwa.
Naye Ramadhani Kidodora mmiliki wa boti za uvuvi katika mwalo wa KIGODECO alisema kuwa baada ya shughuli za uvuvi kufungwa ziwa Tanganyika hali ya mji ni ngumu kifedha kwani mzunguko mkubwa wa fedha umepungua na kutokuwepo kwa viwanda mkoani humo kunafanya mkoa kutokuwa na shughuli mbadala.
Kidodora alisema kuwa shughuli za ziwa Tanganyika zilikuwa zinahudumiwa idadi kubwa ya watu wakiwemo mama lishe, wasafirishaji wa vyombo vya moto na wengine na kwamba kufungwa wa shughuli za uvuvi kumeanza kuonyesha kuwepo kwa tishio la kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu.
Mwisho.
0 Comments