Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dk Doto Biteko,katikati akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mradi wa kituo cha kupoza Umeme cha Ifakara ambao utasaidia kuwa na umeme wa Uhakiki kwa wananchi wa wilaya za Ulanga,Malinyi na Kilombero,kushoto Mkuu wa mkoa wa Morogoro,Adam Malima na kulia ni Balozi wan chi za Umoja wa Ulaya Christine Glau,
Na Ashton Balaigwa,IFAKARA
SERIKALI inakusudia kutekeleza mradi mkubwa wa Umeme wenye thamani ya Sh Bilioni 104 kwaajili ya kuhakikisha Wawekezaji wa Madini katika wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro ili kuwepo na umeme wa uhakika waweze kufanya shughuli za kuchimba madini.
Aidha Serikali inatarajia kutangaza wakati wowote Wilaya ya Ulanga,Malinyi na Kilombero kuwa ni mkoa wa Kitanesco kutokana na umuhimu wa wilaya hizo katika kuzalisha mazao mbalimbali yanayosaidia kukuza uchumi ili uwe na bajeti yake kama mikoa mingine.
Naibu Waziri na Waziri wa Nishati,Dk Doto Biteko,alisema hayo mjini Ifakara wilayani Kilombero wakati akizindua mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme wa uhakika kwa wilaya za Kilombero,Malinyi na Ulanga kilichopo mji wa Ifakara.
Kituo hicho kimejengwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa Ushirikiano na pamoja na Jumuiya ya Ulaya kupitia mfuko wa maendeleo (EDF) kwa gharama ya sh bilioni 24.59 ikiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali za kuondoa umasikini katika kuendeleza kilimo.
Naibu Waziri Mkuu alisema wilaya ya Ulanga ni moja ya wilaya zilizobarikiwa kuwa na madini ya aina tofauti ikiwemo ya Kinywe,madini ya vito (Spinal) hivyo wawekezaji wengi wamekuwa wakijitokeza kuwekeza lakini bado kuna changamoto ya uwepo wa umeme wa uhakika”
Tunataka kujenga mradi mkubwa wa umeme wa zaidi ya sh bilioni 104 ambao utakuwa unajitegemea kwa kupeleka umeme wa uhakika katika migodi yetu ili kuweza kuvutia wawekezaji kutoka nje na tunafanya hivi kwa uzito mkubwa “ alisema Naibu Waziri Mkuu Biteko.
Akizungumzia kuhusu manufaa ya mradi wa kituo cha kupoza umeme cha Ifakara,Naibu Waziri Mkuu alisema utasaidia sasa upatikanaji wa umeme wa uhakika katika wilaya za Kilombero,Ulanga na Malinyi ambazo zilikuwa na changamoto ya kukatika kwa umeme zaidi ya masaa nane kwa siku lakini baada ya mradi huo kukamilika sasa umeme unakatika kwa dakika 46 pale yanapofanyika matengenezo.
Alisema kukamilika kwa mradi huo pia kutawezesha sehemu za biashara na viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo 54 kupata umeme kwa uhakika na kufanya ukusanyaji wa mapato kwa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco ) kuongezeka.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa REA Mhandisi Jones Olotu,alisema wameamua kujenga kituo cha kupoza umeme kilichopo Ifakara kutokana na wilaya hizo kuzalisha kwa wingi zao la mpunga pamoja na miwa ambayo yanasaidia kukuza uchumi wa nchini.
Alisema kutokana na umuhimu wake kwa wilaya hizo tayari vijiji 110 vilivyopo eneo la mradi vimeshapatiwa umeme vilivyobaki 180 baada ya miaka miwili navyo vitakuwa na umeme.
Naye Balozi anayewakilisha nchi za Umoja wa Ulaya,Christine Glau,alisema umoja huo utaendelea kuisaidia Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi yake mbalimbali yakuondokana na umasikini.
Alisema kituo hicho ni miongoni mwa vituo 14 ambavyo wanatarajia kuvijenga hapa nchini ambavyo vitakuwa na thamani ya sh bilioni 600.
Balozi huyo alisema kuwepo kwa umeme huo wa uhakika sasas utaweza kusaidia wakulima wa mpunga kuuza mchele badala ya kuuza mpunga kwa bei ya chini.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Adam Malima,alisema wilaya hizo tatu za Kilombero,Ulanga na Malinyi kwa muda mrefu zilikuwa zikikabiliwa na changamoto ya umeme licha ya kuwa kinara wa uzalishaji wa mpunga na miwa.
Alisema asilimia 70 ya sukari inayozalishawa hapa nchini inatoka mkoa wa Morogoro ambao una viwanda vinne vya kuzalisha sukari
pamoja na kuzalisha mpunga.
Mwisho
0 Comments