Katika kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Familia ambayo uadhimishwa Mei 15, kila mwaka, Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) Wakili Onesmo Olengurumwa amesema changamoto nyingi za kimaadili na kitabia ambazo zimekuwa zikitokea kwenye jamii zimechangiwa na kuyumba kwa 'taasisi ya familia'.
Akizungumza leo na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam ametaja baadhi ya changamoto hizo ambazo zinaweza kuwa zimechangiwa na matokeo ya familia nyingi kuyumba, kati hizo ni pamoja na kuongezeka kwa 'watoto wa mitaani', vijana kujiingiza kwenye vikundi vya uharifu pamoja na kupolomoka kwa maadili.
Amedai kuwa kwa kiwango kikubwa watoto ambao wamekuwa wakitokea kwenye familia imara na kupata malezi bora ni ngumu kujihusisha na tabia zisizo rafiki kwenye jamii kutokana na kuwa na mienendo yao mizuri wamejengewa.
"Faida za kuwa na familia imara yenye amani na upendo kwa watoto ni kubwa sana, kwanza watoto watakuwa salama, sio rahisi watoto kufanyiwa ukatili, watoto watakuwa na maadili mazuri lakini utaona hata idadi ya watoto wa mitaani inapungua"amesema Olengurumwa
Ameongeza kuwa baadhi ya matukio ya ukatili kwa watoto yamekuwa yakichangiwa kwa kiwango kikubwa na 'taasisi ya familia' kuyumba.
Pia Olengurumwa amedai kuwa yapo madhara makubwa yanayoweza kutokea endapo suala la familia halitapewa uzito au umuhimu, ametolea mfano kwamba ikitokea mtoto hajapata malezi ya familia ni vigumu mbeleni kuwa na familia imara yenye upendo na mshikamano.
Aidha kufuatia changamoto hizo ambazo amezibainisha, amesema kuwa siku ya familia inatakiwa kupewa uzito mkubwa kwa kuwa ndio msingi wa jamii bora yenye kuzingatia haki, maendeleo ya kiuchumi, maadili mema na masuala mengine yenye tija.
Amependekeza siku hiyo ikiwezekana ikawe siku ya mapunziko ili kutoa fursa kwa wanafamilia kukutana kutafakari masuala ya kifamilia sambamba na Serikali kuadhimisha kwa kufanya mijadala na mikutano yenye kuleta tija zaidi katika kuboresha na kudumisha 'taasisi ya familia'.






0 Comments