Mkuu wa mkoa wa Songwe Daniel Chongolo akiwa na mkuu wa wilaya ya Mombo Kenan Kihongosi (kushoto )
Na Moses Ng'wat, Momba.
MKUU wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa bwawa la maji la Chiwanda katika kijiji cha Chiwanda, kata ya Nkangamo, Wilayani Momba, unaotekelezwa na serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 1,306,158,637.
Amebainisha hayo, Mei 15 ,2024 baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya Ujenzi wa bwawa hilo, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili Wilayani Momba kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.
Mkuu wa Mkoa Chongolo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha ambazo zinawezesha utekelezaji wa mradi huo mkubwa ambao kukamilika kwake utasaidia wananchi 14,449, pamoja na mifugo 2,609 katika kijiji hicho cha Chiwanda chenye vitongoji saba katika kata ya Nkangamo.
Aidha, Chongolo amewataka wataalamu wa bodi ya maji Bonde la Ziwa Rukwa (LRBWB) na Wakala wa maji mijini na vijiji (RUWASA) Wilaya ya Momba wanaotekeleza mradi huo kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika ifikapo Agosti 30 mwaka huu ili uanze kutoa huduma kwa wananchi hao.
Vile vile ametoa siku 14 kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba kuhakikisha wanawashirikisha wanachi kupanda miti inayohifadhi maji kuzunguka mradi huo.
"Haiwezekani serikali imeleta mradi huu mkubwa halafu sisi tunashindwa kutunza mazingira yake, naomba wananchi mjitokeze kupanda miti ambayo italetwa hapa bure na Wakala wa Misitu (TFS) tena mingine itakuwa ni miti ya matunda ambayo ni faida kwa afya zetu" amesema Chongolo.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa ametoa tahadhari kwa wananchi kuepuka kuingiza mifugo kwenye bwawa hilo, huku akitaka watendaji wa vijiji na kata kuchukua hatua kali kwa wale watakaobainika kuingiza mifugo na kufanya uharibifu.
Kaimu Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Momba, Mhandisi Beatus Katabazi, alisema sababu za serikali kujenga bwawa hilo ni kutokana eneo hilo kuwa na kiasi kidogo cha maji chini ya ardhi.
Alisema hali hiyo ya kiasi kidogo cha maji chini ya ardhi katika eneo hilo kimesababisha miradi mingi ya maji ya visima kushindwa kukidhi mahitaji ya wananchi.
0 Comments