Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Florent Laurent Kyombo ameishauri Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kuboresha mazingira ya biashara maeneo yaliyopo mipakani na Nchi jirani ili kuepusha changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza.
Akichangia hoja kwenye Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara leo Mei 22, 2024 Bungeni jijini Dodoma kwenye kikao cha 31 ametolea mfano eneo la Mtukula ambalo limepakana na Nchi ya Uganda amesema kuwa kumekuwepo na changamoto nyingi ambazo zimepelekea baadhi ya watanzania kuamia upande wa Uganda.
"Mh. Mwenyekiti, ukienda pale Mtukula utashangaa ndani ya kilometa 10 za upande wa Nchi jirani zaidi ya asilimia 70 ya biashara iliyopo kule ni ya watanzania, wamekimbia upande wa Tanzania, ni kwa sababu mazingira yamekuwa ni magumu
Ameongeza "Wizara ya aridhi imeenda pale Mtukula imejenga jengo zu la National Housing, lakini leo ukienda pale wamebaki pale wafanyabiashara wawili wengine wote wameingia upande wa Uganda"
Kufuatia suala hilo ameshauri Serikali kuweka mazingira rafiki ili kuvutia mazingira ya kibiashara yanayovutia yanayoweza kuchochea mapato zaidi, amesema kuwa Serikali inaweza kuwa na utaratibu wa miongozo inayoendana na maeneo husika kwenye mipakani ili kurahisisha mazingira ya kibiashara kuwa rafiki zaidi.
Pia ameshauri kuboreshwa kwa miundombinu hususani ya barabara ambazo zinawezesha wafanyabiashara kufika kiurahisi kwenye nchi jirani zinazopakana na Mkoa wa Kagera, jambo ambalo amedai liongeza pia wigo wa mapato.
Aidha ameishauri Serikali kupitia mamlaka zenye dhamana kusimamia ipasavyo bidhaa feki za vipodozi ambazo zipo sokoni akidai kuwa zahatarisha afya ya wananchi.
0 Comments