Mkoa wa Njombe umetekeleza kwa vitendo agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Kassim Majaliwa ya kufanya mazoezi kila mwisho wa wiki kwa ajili ya afya kwa Taasisi za Serikali ,Taasisi binafsi na Wananchi kwa ujumla.
Utekelezaji wa agizo hilo kwa vitendo umefanyika katika Halmashauri ya Mji Makambako ,Wilaya ya Njombe mkoani Njombe .
Mazoezi hayo ya kukimbia taratibu (Jogging) yameshirikisha Taasisi za Serikali,Taasisi binafsi, Watu binafsi na Vikundi vya Taxas na Wenyeji Makambako Jogging Club (MJC 2022) wenye kauli mbiu ya " Mazoezi kwa afya"
Taasisi za Serikali zilizoshiriki na mazoezi hayo ya kukimbia taratibu ( Jogging) na mazoezi ya viungo ni Jeshi la Polisi Wilaya ya Kipolisi Makambako na Watumishi wa Halmashauri ya Mji Makambako ambao ndio walioratibu mazoezi hayo.
Mazoezi hayo kwa pamoja yalifanikishwa kwa ushiriki mkubwa wa Watumishi wa Halmashairi ya Mji Makambako, Jeshi la Polisi kituo cha Makambako na wenyeji Makambako Jogging Club (MJC 2022)
Upande wao Viongozi wa Makambako Jogging Club (MJC 2022) walitoa wito kwa Wananchi wa Makambako kupenda kufanya mazoezi kwa afya ili kulinda afya na miili yao.
DJ Josee Masekhoo mwalimu wa Jogging na mazoezi kwa kutumia muziki (Aerobics ) alisema lengo la kuanzishwa kwa MJC 2022 ni kutaka Wananchi wote Makambako washiriki kufanya mazoezi.
"Shauku yetu MJC 2022 tunatamani sana kuona kila mtu Makambako anafanya mazoezi walao kwa wiki mara mbili au tatu na hasa kwa kuzingatia kauli mbiu yetu ya " Mazoezi kwa afya" Alisema DJ.Josee .
DJ .Josee alisema mazoezi ni kinga ya magonjwa yote yasiyoambukiza na mazoezi yanaimalisha mwili na viungo badala ya kukaa bila kufanya mazoezi jambo ambalo alidai ni kujilemaza na kuulemaza mwili.
Yona Kayuni " Trainer" Mwalimu wa mazoezi ya viungo kwa upande wake aliongeza kuwa mazoezi ni afya na afya ni mtaji na kuwaasa Wananchi kupenda mazoezi bila kujali umri wala haiba ya Mtu .
"Kauli mbiu yetu ya " Mazoezi kwa afya" inatutaka wote tufanye mazoezi na tuwe na afya njema na tuweze kulijenga taifa letu la Tanzania kwa kujituma kufanyakazi kwa bidii na bila afya huwezi kufanyakazi." Alisema Yona Trainer.
Aliongeza kusema Wana Makambako wote wanakaribisha kufanya mazoezi kwani hakuna kiingilio bali kiingilio ni muda na kufuata ratiba za siku za mazoezi .
Aidha aliweka bayana ratiba ya Makambako Jogging Club kuwa siku ya Jumatatu kukutana ni Uwanja wa Polisi saa 12:00 asubuhi kwa ajili ya mazoezi ya viungo na Jumatano ni Jogging "route "fupi mbio za pole pole km 7 kukutana ni Dama saloon mkabara na lango kuu la kuingilia Kituo cha Polisi Makambako.
Siku ya Alhamis ni mazoezi ya viungo kwa kutumia muziki "Aerobics" Jukwaa la Uwanja wa Polisi Makambako na Jumamosi ni mbio za pole pole " route" ndefu km 10 kukutana ni saa 11:40 alfajiri Dama saloon jirani na geti kuu la kuingia kituo cha Polisi wilaya ya Kipolisi Makambako na kumalizia Uwanja wa Polisi Makambako.
Makambako Jogging Club (MJC 2022) ilianzishwa rasmi Mei 21 mwaka 2022 ndani ya viunga vya mji wa Makambako lengo likiwa kila Mtu kushiriki kufanya mazoezi.
0 Comments