![]() |
| Mwantumu Mgonja Mkurugenzi manispaa ya Kigoma Ujiji |
Fadhili Abdallah,Kigoma
Licha ya mpango wao wa kupiga kura ya kutokuwa na imani naye kushindwa MADIWANI katika baraza la madiwani la manispaa ya Kigoma Ujiji wameonyesha nia ya kutotaka kufanya kazi na Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Ujiji Mwantumu Mgonja wakimtuhumu kushindwa kutekeleza mambo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya halmashauri hiyo.
Madiwani hao wakiongozwa na Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji,Baraka Lupoli kwa kutumia kikao cha baraza la kawaida la madiwani la robo ya nne lililofanyika juzi walikuwa na nia ya kupiga kura ya kutokuwa na Imani na Mkurugenzi huyo katika kikao cha kawaida kilichogeuzwa kuwa kamati ili kujadili masuala ya utumishi kumhusu mkurugenzi huyo.
Hata hivyo mpango huo haukuzaa matunda kwa kile kinachoelezwa kuwa Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye kuingilia kati nia hiyo ya madiwani katika kikao cha kamati kwa ajili ya kujadili masuala ya kiutumishi
![]() |
| Madiwani wa manispaa ya Kigoma Ujiji wakiwa kwenye kikao |
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho cha kamati kilichochukua masaa Matano zinaeleza kuwa Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye alitumia ushawishi mkubwa kuwataka madiwani hao kujadili changamoto zinazojitokeza na kuzifanyia kazi kwa kila upande badala ya kumuazimia mkurugenzi na kutaka aondolewe.
Awali kabla ya kufikia huko baada ya kufungua kikao na kuthibitisha ajenda Meya wa manispaa ya Kigoma, Baraka Lupoli aliomba wajumbe wa baraza kuanza kujadili ajenda ya mapato na matumizi na masuala ya kiutumishi na hali ya uendeshaji wa halmashauri na baada ya hapo ndipo ajenda nyingine ziendelee.
Baadhi ya Madiwani ambao ni wajumbe wa baraza hilo akiwemo diwani wa kata ya Bangwe , Hamisi Betese,diwani wa kata ya Buhanda,Kilahumba Rutuli na Himidi Omari wa kata ya machinjioni
walikubaliana kwamba suala hilo liletwe kwenye baraza ili lijadiliwe na madiwani wote kwa sababu mambo mengi yanayoamuliwa na kamati ya fedha na uongozi hayatekelezwi na Mkurugenzi ameonekana kutotekeleza maagizo na maelekezo hayo kwa makusudi.
![]() |
| Meya wa manispaa ya Kigoma Ujiji Baraka Lupoli (aliyesimama) akiwa na Mkurugenzi wa manispaa hiyo Mwantumu Mgonjwa (aliyekaa kulia) |
Hata hivyo jambo hilo lilipata upinzani mkubwa kutoka kwa Afisa utumishi wa manispaa hiyo, Idrisa Naumanga na Mkuu wa kitengo cha sheria, Less Majala ambao kwa wakati tofauti walitaka ajenda hiyo kutojadiliwa kwani haikupita kwenye kamati ya fedha na uongozi hivyo ni lazima irudi huko kwanza ndiyo iletwe kwenye baraza jambo ambalo linaweza kujadiliwa kikao kijacho na siyo hicho.
Kutokana na mvutano mrefu na hatimaye kusomwa kwa kanuni hiyo Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Baraka Lupoli alitoa taarifa ya baraza kujigeuza kuwa kamati hivyo kuomba watu wote kutoka nje ambapo madiwani na baadhi ya wakuu wa idara ndiyo watakabaki ndani kuendelea na kikao cha kamati hivyo watu wote walitoka nje.
Baada ya masaa matano ya kikao cha kamati Meya wa manispaa ya Kigoma Ujiji, Baraka Lupoli aliomba watu wote kurudi kwenye baraza na akatoa tamko la kufungwa kwa kikao cha baraza akieleza kuwa yapo masuala ya kiutimishi yaliyojadiliwa ambayo yatapelekwa kwenye mamlaka za kiutumishi zinazohusika.
Aidha baada ya kufungwa kwa kikao cha baraza waandishi wa Habari waliomba Meya Lupoli kutoa taarifa kwa ufupi kilichoamuliwa kwenye baraza hasa suala la kumuazimia mkurugenzi ambapo alisema kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo kwani azimio la kikao cha kamati suala hilo kupelekwa kwenye mamlaka za kiutumishi kwa watendaji wanaohusika.








0 Comments