Header Ads Widget

KAILIMA ATOA NENO KWA VYAMA VYA SIASA KUHUSU DAFTARI



Fadhili Abdallah,Kigoma

 

TUME huru ya Taifa ya uchaguzi (INEC) imetangaza kuzinduliwa kwa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura Jula Mosi mwaka huu huku likitoa maelekezo kwa vyama vya siasa kuweka mawakala kusimamia zoezi hili huku vyama hivyo vikitakiwa kugharamia posho za mawakala wao.

 

Mkurugenzi wa Tume huru ya uchaguzi Tanzania, Dk.Ramadhani Kailima alisema hayo akizungumza na waandishi wa Habari mjini Kigoma kuhusiana na maandalizi ya uzinduzi wa zoezi hilo utakaofanyika mjini Kigoma katika manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajia kuwa mgeni rasmi.



Kailima alisema kuwa zoezi hilo la uboreshaji la daftari la wapiga kura  linafanyika kwa kuandikisha wapiga kura wapya wenye umri wa miaka 18 na Zaidi, kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa awali na ambao wamehama kutoka mkoa au wilaya moja kwenda nyingine waweze kuhamisha taarifa zao,kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi kuharibika  na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa Tanzania na kifo.

 

Kutokana na hilo Kailima ametoa wito kwa vyama vyote vya siasa kupeleka majina ya mawakala wao kwenye vituo vyote kwa siku zote zoezi litakapokuwa linafanyika na kwamba Pamoja na hilo vyama hivyo vya siasa vinapaswa kugharamia nauli,chakula na posho kwa mawakala wao watakaokuwa wakifanya kazi ya kuhakiki wapiga kura wanaoingizwa kwenye daftari ndiyo wanaostahili.

 


Akizungumzia uboreshaji huo wa Daftari la kudumu la wapiga kura  Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Vijana Kigoma (YAAPA), Alex Luoga ameiomba INEC itoe vibali kwa wingi kwa mashirika kutoa elimu ya uraia na upigaji kura ili kuwafanya watu wengi kujua zoezi hilo na umuhimu wake lakini pia kutoa msisitizo kwa vijana kushiriki kwenye uandikishaji na zoezi la uchaguzi mzima.


Sambamba na hilo Luoga amesema kuwa tume huru ya uchaguzi inapaswa kugharamia mawakala wa vyama vya siasa wanaoshiriki kwenye zoezi la uboreshaji wa daftari hilo kwani wanafanya kazi kuisaidia tume hiyo ya uchaguzi hasa kuhakiki wapiga kura wanaoapaswa kuandikishwa na kufanyiwa maboresho.

 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI