NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana na wenye Ulemavu, Patrobas Katambi (Mb) amekutana na kufanya kikao na kamati ya maandalizi ya sherehe za Mei Mosi wakiongoza na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Chtistian Makonda pamoja na Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Aprili 20, 2024.
Katika kikao hicho Katambi amewapongeza wajumbe wa kamati hiyo ya maandalizi kupitia Sekretarieti ya Mkoa wa Arusha ikiongozwa na Mkuu wa mko na Katibu Tawala wa mkoa huo, kwa kazi nzuri na mipango mizuri iliyofanyika mpaka sasa, jambo ambalo linatia moyo kuwa Mei Mosi 2024 itakuwa ya tofauti.
“Nimefarijika sana kwa kazi nzuri na kubwa ya maandamizi iliyofanyika mpaka sasa, inaonesha ni jinsi gani wanakamati wanajituma licha ya majukumu mengi ya kikazi waliyo nayo, endeleeni na moyo huo mpaka Siku yenyewe ya Mei Mosi, tukampambe Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan”
Amewataka wajumbe wa kamati ya maandalizi kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kukamilisha shughuli walizopangiwa kwa wakati na hatimaye kufikia malengo ya Siku maalum ya Wafanyakazi Duniani ambao ndio wajenzi wa Taifa la Tanzania.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema maandalizi yanaendelea vizuri na kila Kamati inafanya kazi kikamilifu na kuhakikisha kuwa sherehe hizo zinafanana
Aidha, Makonda amewasihi wananchi wa mkoa wa Arusha na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo, ambayo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika kikao hicho pia wameshiriki Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wakioongozwa na rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, Wakuu wa Wilaya za mkoa wa Arusha, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Missaile Musa, Makamishna wa Kazi Wasaidizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri zake.
0 Comments