Header Ads Widget

RC DENDEGO AZINDUA CHANJO YA SARATANI SINGIDA, ATAKA WATOTO WA MITAANI NAO WAFIKIWE

Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA

MKUU wa Mkoa wa Singida,Halima Dendego,amezindua kampeni ya chanjo dhidi ya Saratani ya Mlango wa Kizazi (HPV) ambayo mkoa umelenga kuchanja wasichana 178,144 wenye umri kati miaka 9 hadi 14 huku akisisitiza watoto wote wafikiwe wakiwamo wa mitaani.


Akizungumza na wananachi na wanafunzi katika kata ua Kisaki Halmashauri ya Manispaa ya Singida kabla ya kuzindua chanjo hiyo leo (Aprili 22, 2024),amesema chanjo hiyo ni mpango wa serikali wa kuwalinda wanawake ili kirusi kinachosababisha ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi kisiweze kuwapata na kuleta madhara.

"Serikali imewekeza kwa watu wake maana huwezi kuwa ba barabara nzuri,shule bora kama wati wake ni wagonjwa,na kama mnavyofahamu ugonjwa wa saratani bado ni changamoto unapompata mwanamke mara nyingi ni kifo,kwa hiyo mtu anapopewa chanjo hii maana yake anawekewa askari wa kumlinda," amesema Dendego.


Dengedo amesema timu zote za kampeni zihakikishe zinawafikia watoto wote kwenye shule za serikali na binafsi, migodini na watoto wa mitaani kwani chanjo hii inatolewa bure na haina madhara yeyote kwa wanaopewa kama ambavyo waliowahi kupewa wametoa ushuhuda.


Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa serikali kupitia Wizara ya Afya na Wizara Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imewekeza fedha nyingi hivyo jukumu la wazazi na walezi wenye watoto wao waliofikisha umri kuanzia miaka 9 hadi 14 kutoa ushirikiano ili wakapatiwe chanjo hiyo.


"Itakuwa ni aibu kwa mkoa ambao Mkuu wa Mkoa ni mwanamke,Katibu Tawala wa Mkoa ni mwanamke na Mganga Mkuu wa Mkoa ni mwanamke halafu wasichana wasichanjwe,nataka kuona Mkoa wa Singida unakuwa namba moja kwa kila jambo,namba moja haina fitina wala majungu,"amesema Dendego.


Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida,Dk.Fatuma Mganga,amesema kitendo kinachofanywa na serikali cha kutoa chanjo hii ni uwekezaji kwa wananchi wake hususani wanawake ili wawe na afya njema na hivyo washiriki vyema katika shughuli za uzalishaji mali.


"Uwekezaji huu ili uwe na tija ni muhimu kwa walengwa wote kuhakikisha wanapata chanjo,kwa REO (Afisa Elimu Mkoa) hakikisha wanafunzi wote wenye umri wa miaka 9 hadi 14 wanapata chanjo na kipindi hiki ndio cha muhimu kusisitiza suala la mahudhurio kwa wanafunzi ili walengwa wote wapate chanjo," amesema Dk.Mganga.


Dk.Mganga amesema pamoja na vituo vilivyotengwa kwa  ajili ya kutolea chanjo lakini pia maeneo mengine kama kwenye machimbo ya madini yafikiwe ili wasichana waliopo maeneo hayo nao wapewe chanjo.


Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Victorina Ludovick, amesema chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi imeanza kutolewa kuanzia Aprili 22 hadi 26, mwaka huu ma itaendelea kutolewa hadi Disemba mwaka huu na walengwa ni wasichana wenye umri wa miaka 9 hadi 14.


Amesema chanjo hii inatolewa kwa wanawake kwasababu Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi ambazo zinapoteza wanawake wengi kutokana na ugonjwa wa saratani ya lango wa kizazi ambao huambukizwa kwa njia ya kujiamiana.


"Chanjo hii imeanza kutolewa kwa dozi moja badala ya mbili kwasababu tafiti zinaonesha kuwa dozi moja tu inaweza kukinga maradhi hayo kwa mwanamke na ifikapo Januari 2025 chanjo hii itaanza kutolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 9 tu," amesema.


Aidha, Ludovick alisisitiza wanawake kufanya uchunguzi wa afya zao kupitia vifaa vya kitabibu ili kugundua kama wana virusi vya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi kwa hiyo itasaidia kupata matibabu haraka.


Naye Mtaalam kutoka Wizara ya Afya, Nelson Kamuhanda,amesema chanjo hii ambayo ilianza kutolewa tangu 2018 serikali imeanza kutoa chanjo tena baada kubaini mikoa mingi ilionekana ipo chink katika utoaji wa chanjo isipokuwa Mkoa wa Kigoma.


Amesema mwaka 2018 chanjo hiyo ilikuwa inatolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 tu kwasababu hakukuwa na chanjo (dozi) ya kutosha lakini kwa hivi sasa chanjo ipo ya kutosha.


"Saratani ya Mlango wa Kizazi ni moja ya saratani kuu nne ambazo zinasababisha kifo hivyo serikali ikaona itoe chanjo kuwakinga wanawake," amesema Kamuhanda.


Mkuu wa Wilaya ya Singida,Godwin Gondwe,amesema katika uzinduzi huo wanafunzi 410 kutoka katika shule za kata ya Kisaki watapewa chanjo hiyo na kwamba wamejipanga kuhakikisha wilaya hiyo inashika nafasi ya kwanza kwa kutoa chanjo wa walengwa wengi.


MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI