NA JOSEA SINKALA, ILEJE SONGWE.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mheshimiwa Daniel Chongolo, ameanza ziara ya kikazi katika Wilaya ya Ileje kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo na kujitambulisha kwa wananchi tangu alipoteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mkuu wa Mkoa huo.
Chongolo ameanza ziara hiyo jumapili hii (Aprili 28, 2024) kwa kutembelea shule ya wasichana ya Sekondari Ileje (Ileje Girls school) ambayo imefikia kidato cha pili na inatarajiwa kufika kidato cha sita ambapo pia kuna mradi wa vyumba 11 vya madarasa.
Akizungumza na wananchi na ujumbe alioambatana nao, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Daniel Chongolo ameelekeza mafundi na wasimamizi kuongeza kasi ili kuhakikisha ujenzi wa vyumba hivyo unakamilika kufikia Juni mosi mwaka huu (2024).
Naye mkuu wa Wilaya ya Ileje Mhe. Farida Mgomi, ameishukuru Serikali kuu kwa uidhinishaji mabillion ya fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali Wilayani kwake ikiwemo kwenye sekta ya Elimu, afya, barabara na maji akiahidi fedha hizo kuendelea kusimamiwa ili kufanya kazi iliyokusudiwa kwa maslahi ya umma.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa, ametembelea na kukagua shughuli zinazofanyika katika mpaka wa Tanzania na Malawi wa Isongole Wilayani Ileje ambapo amepokea kero mbalimbali ikiwemo ukosefu wa huduma ya maji safi.
Akijibu hoja hiyo Meneja wa Wakala wa usambazaji maji vijijini (RUWASA) Wilaya ya Ileje Mhandisi Andrew Tesha amesema tayari wanaendelea kushughulikia tatizo la ukosefu wa maji safi mpakani hapo na wataanza kutekelezwa mwezi mmoja baada ya kupata fedha hivi karibuni.
Sanjari na hayo, Chongolo ameviagiza vyombo vinavyohusika hasa Jeshi la Polisi Mkoani Songwe, kuhakikisha linapambana na vitendo vya utoroshaji wa bidhaa kwa njia za panya hususani mbolea jambo ambalo ni uhujumu uchumi kwa kutorosha pembejeo hizo kwenda kuuza nje ya nchi.
Pamoja na hayo amekagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya msingi Ipapa na baadaye kukagua ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao Wilayani Ileje ambapo katika maeneo yote Mkuu huyo ameonekana kutokuwa mtu wa maneno badala yake anaahidi kuwa mtu wa vitendo zaidi kwa kufuatilia miradi ya Serikali kuhakikisha inakwenda mbele kupitia fedha zinazotengwa na kutolewa na Serikali kuu pamoja na zile za mapato ya ndani ikiwemo katika Wilaya hiyo ambayo ni mpakani mwa Tanzania na Malawi.
Hii ni ziara ya kwanza ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe Daniel Chongolo kujitambulisha kwa wananchi na kutembelea miradi mbalimbali ambapo pia jumapili hii (Aprili 28, 2024) ameshiriki ibada katika Kanisa la KKKT Dayosisi ya Konde Usharika wa Tunduma ambapo amezindua ukumbi mkubwa uliojengwa ili kuwa kitega uchumi cha Kanisa katika kukuza uchumi wake na Taifa kwa ujumla akiongozwa na Mkuu wa Kanisa hilo Mch.Dkt. Alex Malasusa.
0 Comments