Header Ads Widget

MAAFA YA FERI YA MSUMBIJI: "NILINUSURIKA, LAKINI NILIPOTEZA WATU 17 WA FAMILIA YANGU"

 "Sijui niliwezaje kunusurika - siwezi kuogelea," anasema Muaziza Ambaraje.Alikuwa ndani ya mashua ya kujitengenezea wakati maafa mabaya zaidi ya baharini nchini Msumbiji katika kumbukumbu ya hivi majuzi yalipotokea Jumatatu.

Mwanamke huyu mwenye umri wa miaka 47 amekuwa akitumia mara kwa mara mashua hiyo kwa safari zake kati ya Lungá, ambako alizaliwa, na Kisiwa cha Msumbiji anakoishi.

"Hakuna wimbi lililotushtua , hatukugonga miamba yoyote, na wala mbao za mashua hazikuwa zimelegea," anakumbuka."Maji yaliingia ndani kwa sababu ilikuwa imejaa watu wengi - watu wengi waliingiwa na hofu na kuanza kuruka baharini."

Kisha, Bi Ambaraje anaelezea kushuhudia mrundo mkubwa wa kutisha wa watu waliokuwa hai na waliokufa , alipokuwa akijitahidi kuelea. Zaidi ya watu 100 walikufa katika mkasa huo siku ya Jumatatu, wakiwemo watu 17 wa familia yake.

Mama yake, baba yake, nyanya yake, na wapwa zake wote walifariki, anasema Bi Ambaraje. Hawezi kufikiria sababu yoyote ya yeye kuepuka kifo zaidi ya rehema ya Mungu.

Walikuwa wakienda soko maarufu la kila wiki la Kisiwa cha Msumbiji kabla ya Eid, anasema Bi Ambaraje, katika kile kilichokusudiwa kuwa wakati wa sherehe katika sehemu hii yenye Waislamu wengi nchini humo.

"Nilihisi nimeishiwa nguvu kabisa ndani ya mwili wangu," anakumbuka Momade Issufo, ambaye alikimbia kuokoa watu Jumatatu mara tu aliposikia habari za ajali ya meli.

"Niliona maiti zikiwa zimerundikana ufukweni - wengine walikuwa watoto wenye umri wa miaka mitatu. Watu walikuwa na hofu.

Sikuwa na la kufanya - kama binadamu ilibidi nisaidie. Bado kulikuwa na watu kwenye mashua za uokoaji, kwa hivyo tulisafirisha miili yao kwenye lori langu hadi kwenye nyumba za jamaa zao."

Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 44 anasema binamu yake aliyekuwa mjamzito alikuwa miongoni mwa waliofariki. Tukio hilo limemfanya ahisi kuwa mwenye msongo wa mawazo na kushindwa kufanya kazi.

Wavuvi kwenye Kisiwa cha Msumbiji boti kadhaa zilisaidia kubeba watu hai na wafu hadi ufukweni kwenye Kisiwa cha Msumbiji 

Bw Issufo anaitaka serikali ya Msumbiji kujenga daraja jipya kutoka bara hadi kisiwani, eneo la Urithi wa Dunia wa Unesco, ili watu wasitegemee mashua hizo hatari.

Maelfu ya mashua za uvuvi zinafanya kazi kinyume cha sheria kama feri kwenye ufuo wa pwani wa kilomita 2,750 (maili 1,708), kwa idhini ya serikali yenyewe.

Abiria wamesema kwamba waendeshaji wasiodhibitiwa mara nyingi hupakia mashua wasafiri wengi ili kuongeza faida yao.Kwa nini Msumbiji imeruhusu hili kutokea? Je, waathiriwa wa Jumatatu watapata fidia gani? Na mamlaka itazuiaje maafa kama hayo kutokea tena?

Hata hivyo, afisa wa eneo la mkoa wa Nampula, Katibu wa Jimbo Jaime Neto, baadaye aliongea na mwanahabari kwamba usafiri, chakula na msaada wa kisaikolojia unatolewa, na majeneza kwa ajili ya watu waliofariki yalikuwa yametolewa.

Bado hakuna mazungumzo kuhus fidia au msaada wa kifedha.Siku tatu za maombolezo ya kitaifa zinakamilika siku ya Ijumaa, na uchunguzi unazinduliwa ili kuelewa chanzo cha ajali hiyo na kutoa mapendekezo.

Maelezo ya awali ya serikali kuhusu mkasa huo wa Jumatatu ni kwamba watu waliojawa na hofu walikuwa wakikimbia bara kwa wingi, baada ya taarifa za uongo kusambazwa kwa nia mbaya zikiwaambia ni lazima waende kisiwa cha Msumbiji kuepuka mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu unaoendelea.

Akiwazuru wafiwa siku ya Jumatano, Rais Filipe Nyusi alilaani "imani mbaya" waenezaji wa habari potofu ambao "huzua hofu na vitisho miongoni mwa watu".

Ajali za mashua si jambo la kawaida nchini Msumbiji lakini ni nadra watu wengi kufariki.Idadi ya waliofariki bado inazua utata

Baadhi ya waliofariki wamezikwa wawili kwenye kaburi katika kisiwa cha Msumbiji

Afisa mmoja wa eneo hilo alisema watu 115 walifariki, idadi kubwa zaidi ya 98 iliyoripotiwa na serikali kuu.

Ibrahim Momade Munheti, kiongozi wa jamii ya Jembesse, pia alisema watu 150 walikuwa kwenye mashua hiyo ilipozama. Lakini serikali ilisema idadi ya waliokuwemo inakaribia 130.

Imani ya Kiislamu inahitaji mazishi ya haraka, na wengi wa waliofariki katika ajali hiyo tayari wamezikwa katika Kisiwa cha Msumbiji - baadhi yao wakiwa wawili kaburini.

Kwa wale waliobaki , sasa wana hisia za huzuni ya kuwapoteza wapendwa wao, iliochanganyika na shukrani kwa ajili ya maisha yao wenyewe.

"Wakati wangu ulikuwa bado haujafika - ilikuwa ni amri ya Mwenyezi Mungu," anasema Muaziza Ambaraje.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI