Header Ads Widget

KAYA 34 WILAYANI RUNGWE HATARINI KUKUBWA NA MMOMONYOKO WA UDONGO

  




Na  Matukio Daima Media ,Rungwe 

KUTOKANA na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo tofauti Wilayani Rungwe mkoani Mbeya Kaya 34 zipo hatarini kukubwa na mmomonyoko wa udongo huku Kaya saba tayari zikiwa zimeathiriwa na  hivyo kutakiwa kuhama maeneo hayo ili kuepuka  athari ambazo zinaweza kujitokeza.


Kauli hiyo imetolewa  April  19  ,2024  wakati Mkuu wa wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya  Mhe.Jaffar Haniu alipoambatana na Kamati ya Maafa Wilaya  kutembelea na kujionea athari zinazoendelea kujitokeza kufuatia kukatika kwa mawasiliano ya barabara ya Kapugi-Lyenje kupitia mto Kiwira.


Haniu  akiwa na kamati ya ulinzi na usalama wilaya ameweza kukagua makazi ya  wananchi  wa kijiji cha  Lyenje yaliyoathiriwa na mvua hizo pia kutembelea maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Kambi ya muda ya wananchi walioathiriwa .


"Mvua hizi zinazoendelea kunyesha  karibu nchi nzima zinaendelea kuleta  athari kubwa hivyo kupelekea ardhi kuleta mmeng'enyo ambao umechangia barabara muhimu kwa uchumi wa Rungwe kukatika "amesema Haniu.


Hata hivyo Haniu amezitaka kaya Saba  wakazi wake wanaotakiwa kuhama  wahame mara moja na kujihifadhi katika eneo maalumu lililotengwa katika katika kijiji cha Lyenje.


Aidha amesema barabara iliyoathiriwa ni kiungo muhimu  cha usafirishaji wa  mazao ya Kahawa, ndizi, parachichi na mahindi kutoka upande mmoja kwenda mwingine huku mashamba ya mbalimbali kuathiriwa.


Bonde la mto kiwira ni maarufu kwa kilimo cha Kahawa,  Migomba na Mahindi  lakini kwa hatua hii wakulima wametahadharishwa kuendelea  kuwa makini ili kujiepusha na maafa yanayoweza kujitokeza.


Mmomonyoko wa udongo umekata barabara na miamba yake kufukia mto kiwira ambao humwaga maji yake katika Ziwa Nyasa.


Hata hivyo Mkuu huyo wa wilaya  ameeleza kuwa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) kuendelea kufanya utafiti wa namna bora ya kurejesha mawasiliano ili wananchi waendelee kunufaika na matunda ya nchi yao.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI