Header Ads Widget

IDADI YA WAVUVI WADOGO YAONGEZEKA





Na Hamida Ramadhan Matukio Daima App Dodoma

KATIKA kipindi cha mwaka 1961  1988 shughuli za uvuvi katika maeneo yote ya uvuvi nchini zilikuwa zikifanywa na wavuvi wadogo na idadi ya wavuvi imeongezeka kutoka wavuvi 75,621 mwaka 1995 waliokuwa wanatumia vyombo vya uvuvi 22,976 hadi wavuvi 198,475 waliotumia vyombo 58,820 mwaka 2023. 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdullah Ulega ameyasema hayo leo jijini hapa wakati wa mkutano na waandishi wa Habari kuelekea mafanikio ya sekta ya Mifugo na Uvuvi kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano. 

Aidha amesema, kiasi cha samaki kilichozalishwa na nguvu hiyo ya uvuvi (wavuvi na vyombo)   kiliongezekakutoka tani 255,900.74 za samaki zenye thamani ya TShs.  70,467,575.96 mwaka 1995 hadi tani 479,976.6 zenye thamani ya shilingi trilioni 3.4 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 87.56. Kwa ujumla uzalishaji wa samaki umeonekana kuongezeka hali inayoashiria kuboreka kwa shughuli za uvuvi na maisha ya wavuvi wadogo nchini.


Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na  Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewezesha utekelezaji wa mradi mkubwa wa kielelezo wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi  Kilwa Masoko wenye thamani ya shilingi bilioni 289.5 na tayari kiasi cha shilingi bilioni 106.23 kimetolewa. 


Ujenzi umefikia asilimia 52 na ajira za moja kwa moja 278 zimetolewa kwa wananchi katika eneo la mradi.


" Kukamilika kwa ujenzi huo kutawezesha: Meli za uvuvi zinazovua katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Tanzania (EEZ) na Bahari Kuu kutia nanga na kushusha samaki wanaolengwa na wale wasiolengwa; kuchochea uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya uvuvi; kuimarisha biashara ya mazao ya uvuvi kwenda nje ya nchi; na kuchangia katika pato la Taifa," Amesema Waziri Ulega. 

Amesema Sekta ya Mifugo ni miongoni wa Sekta za Kiuchumi na Uzalishaji ambayo inatoa ajira kwa wananchi wengi wa Tanzania, Sekta ya mifugo ilikua kwa asilimia 5.0 na mchango wa Sekta katika pato la Taifa (GDP) ulifikia asilimia 6.7 kwa mwaka 2022. 


Amesema Idadi ya mifugo nchini ngombe milioni 36.6, mbuzi milioni 26.6 na kondoo milioni 9.1.


Pia, kuku waliopo ni milioni 97.9 ambapo kuku wa asili ni milioni 45.1, kuku wa kisasa milioni 52.8 na nguruwe ni milioni 3.7.

Tasnia ya Nyama 

Amesema,Uzalishaji wa nyama umeongezeka kutoka tani 97,000 mwaka 1964 hadi tani 738,166 mwaka 2023 hii imetokana na kuongezeka kwa viwanda vya kusindika nyama kutoka kiwanda kimoja mwaka 1964 (Tanganyika Parkers) kilichokuwa na uwezo wa kuchinja ngombe 800 kwa siku hadi viwanda 11 vyenye uwezo wa kusindika tani  337 kwa siku.  


Amesema Kwa kipindi cha miaka mitatu (3) ya hivi karibuni, Mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 1,774 mwaka 2020/21 hadi kufikia tani 14,701 mwaka 2022/23. Hivyo kufanya jumla ya tani 35,297 zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 146.43 zilizouzwa nje ya nchi. 

Tasnia ya Maziwa 

Uzalishaji wa maziwa umeongezeka kutoka lita 334,000 mwaka 1964 hadi lita bilioni 3.4 mwaka 2022/2023 na usindikaji wa maziwa umeongezeka kutoka wastani wa lita 41,026,000 kwa mwaka 1964 hadi wastani wa lita milioni 75.9 kwa mwaka 2023. 


Aidha, Viwanda vya kusindika maziwa pia vimeongezeka kutoka viwanda saba (7) vya umma mwaka 1974 hadi kufikia viwanda vya sekta binafsi 105 mwaka 2023.


Amesema Wizara pia imekuwa na ushirikiano na sekta binafsi katika kukuza sekta ya maziwa nchini. Kwa mfano Shirika la Heifer International limeweza kuimarisha mnyororo wa thamani kwa kuwapatia wafugaji wadogo kote nchini jumla ya mitamba bora wa maziwa 282,000, kuku 62,000 na kondoo 57,200 na kujenga vituo 22 vya kukusanyia maziwa vyenye uwezo wa kukusanya lita 70,000 za maziwa kwa siku. 


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS