Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
MKUU wa Mkoa wa Singida,Halima Dendego,amekabidhiwa rasmi mkoa huu huku akisema hapendi kusikia neno changamoto katika maisha yake hivyo watendaji wajipange vizuri katika utendaji wao wa kazi kwa kuhakikisha wanatafuta majawabu ya kero na changamoto zinazowakabili wananchi.
Akizungumza leo (Machi 12,2024) katika hafla baada ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida,Peter Serukamba ambaye amehamishiwa Mkoa wa Iringa,amesema ofisi yake itakuwa wazi kwa kila mtu lakini kwa watendaji hadi wafike kwake wawe wamejipanga sawa sawa.
"Mimi dada yenu mnayenifahamu sina neno linaloitwa changamoto katika maisha yangu na sio kwamba sijawahi kupata changamoto hapana,na sio kwamba changamoto hazipo ila kama Mungu ametuumba tuna akili kuliko kiumbe chochote kile kwanini tushindwe na changamoto,pale kwenye changamoto tutafute majawabu iwe usiku au mchana,liwe jua au mvua majawabu lazima yapatikane," alisema.
Dendego alisema katika utendaji wake atatumia muda mwingi kwenda vijijini kusikiliza kero na kuzitafutia ufumbuzi ili wananchi waendelee kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake.
"Ofisi sio sehemu yangu ila atakuwa RAS (Katibu Tawala wa Mkoa) mimi siku zote nitakuwe nakwenda vijijini kusikiliza kero na changamoto na kuzitafutia majawabu ili wananchi waendelee kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali," alisema.
Dendego alisema amekuja Mkoa wa Singida kwa ajili kuja kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kuleta maendeleo ili kutekeleza ilani ya uchaguzi.
"Nimetoka Iringa kwenye mkoa ambao una uchumi mkubwa,niliipokea Iringa ikiwa na takwimu za juu kiuchumi na kwakweli nilikuwa na changamoto kwamba mbona hizi takwimu zipo juu sana nisije nikatoka hapa nikazishusha lakini namshukru Mungu zilipanda maradufu sana," alisema.
Alisema amekuja katika Mkoa wa Singida ambao ameambiwa kuna changamoto lakini anamshukru Peter Serukamba Mkuu wa Mkoa Iringa amefanya kazi nzuri ambapo muda wote alikuwa akimuona yupo vijijini kusikiliza kero za wananchi na kuzipapatia ufumbuzi.
"Mimi sina shaka Mhe.Peter Serukamba najua umeshanicholea msingi kazi yangu mimi ni kupandisha msingi,"alisema Dendego.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa,Peter Serukamba alisema anafurahi kuondoka Singida huku akiwa ameacha alama katika utendaji ambayo ni pamoja na kupandisha kiwango cha matumizi ya mbolea kutoka tani 2200 hadi kufikia zaidi ya tani 6000.
Alisema jambo jingine analojivunia nalo ni kukomesha mauaji ya watu ambayo yalikuwa yakijitokeza mara kwa mara katika Wilaya ya Manyoni.
"Naondoka nikiwa na moyo mzito na moyo wa furaha,naondoka kwenye mkoa ambao pato la uchumi wa mkoa ni wa tatu kutoka mwisho nakwenda mkoa ambao kiuchumi upo juu,"alisema.
0 Comments