Header Ads Widget

MIAKA 60 YA MUUNGANO, MAFANIKIO YAONEKANA KWENYE SIASA, KIJAMII, KIUCHUMI, MAZINGIRA

 



Na Hamida Ramadhan Matukio Daima App Dodoma


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais  Muungano na Mazingira Dkt, Selemani Jafo amesema kuwa katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar mafanikio makubwa yamepatikana katika nyanja ya Siasa, huduma za kijamii ulinzi na usalama, ,Kiuchumi na mafanikio ya Kimazingira. 


Pia mafanikio hayo yanaenda sambamba na elimu, afya, maji, barabara, umeme, utoshelezi wa chakula pamoja na  ustawi wa jamii kwa ujumla. 


Waziri Jafo ameeleza hayo leo jijini hapa kwenye kikao na waandishi wa habari kilicholenga kutoa taarifa kwa umma kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya Ofisi ya Makamu wa Rais. 


Amesema Muungano kudumu ni kutokana na utashi wa dhati wa kisiasa waliokuwa nao Waasisi wa Muungano ambao uliwezesha vyama vya siasa vya TANU na ASP kuungana na baadaye kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM) tarehe 5 Februari, 1977.


Kuunganishwa kwa vyama hivyo kuliongeza ari ya umoja na ushirikiano baina ya watu wa Tanganyika na Zanzibar na Muungano wa vyama hivyo umekuwa ni nguzo muhimu katika kujenga mfumo wa kuwa na vyama vya siasa vya kitaifa na hivyo kukuza demokrasia, uhuru wa kutoa maoni na uwazi katika uendeshaji wa shughuli za kisiasa. 


Kwa upande wa huduma za elimu, Shule za Msingi zimeongezeka kutoka shule 3,270 mwaka 1961 hadi shule 20,562 mwaka 2024. 


Amesema Kati ya hizo, shule za Serikali ni 18,012 na za binafsi ni shule 2,550 Shule za Sekondari nazo zimeongezeka kutoka shule 41 mwaka 1961 hadi shule 6,511 mwaka 2024,Kati ya hizo, shule 4,892 ni za Serikali na 1,619 ni za binafsi. 


Kwenye Huduma za afya zimeendelea kuimarika kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kipindi chote cha Muungano Kutokana na uwekezaji huo, vituo vya kutolea huduma za afya ngazi zote vimeongezeka kutoka vituo 1,343 mwaka 1960 hadi vituo 9,662 mwaka 2024. 


Ameeleza Kati ya vituo hivyo, Zahanati ni 8,043; Vituo vya Afya 1,176; Hospitali za Halmashauri 171; Hospitali zenye hadhi ya Wilaya 182; Hospitali za Rufaa za Mikoa 28; Hospitali zenye hadhi ya Mkoa 34; Hospitali za Rufaa za Kanda 5; Hospitali zenye hadhi ya Kanda 11; Hospitali maalumu 6; Hospitali ya Taifa 1; na Hospitali Maalumu za Taifa 6. 



"Mfanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano ni kuimarika kwa upatikana wa huduma za maji, umeme na mtandao wa barabara. Upatikanaji wa maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 32 mwaka 2000 hadi asilimia 77 mwaka 2022," Amesema


Katika kipindi chote cha miaka 60 ya Muungano Serikali zetu mbili zimeendelea kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wananchi wa pande zote mbili kufanya kazi kwa uhuru na amani. Hali hii imewezesha nchi yetu kuendelea kujitosheleza kwa chakula ambapo hali ya utoshelezi wa chakula imeongezeka kutoka asilimia 90 mwaka 2000 hadi asilimia 124 mwaka 2022.



Vile vile, udugu na uhusiano wa wananchi umeendelea kuimarika ambapo wananchi wa pande zote mbili wameungana katika misingi ya ndoa na kujenga urafiki katika uendeshaji wa shughuli za kibiashara na kijamii Hali hii inawezesha Watanzania kuwa na uhuru wa kuishi katika eneo lolote la upande wa Muungano, kupunguza migawanyiko ya kijamii na kuondoa hisia za ukabila na ubaguzi miongoni mwao.


MAFANIKIO YA KIUCHUMI


Amesema Tangu kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 Tanzania imepata mafanikio ya makubwa kiuchumi.


 Amebainisha kuwa takwimu zinaonesha kuwa mwenendo wa ukuaji wa uchumi katika kipindi cha miaka 60 umekuwa ni wa kuridhisha ambapo Pato Ghafi la Taifa limeendelea kukua na kufikia shilingi trilioni 170.3 mwaka 2022 kutoka shilingi trilioni 156.4 mwaka 2021.


Aidha, Pato la Taifa kwa mtu limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia wastani wa shilingi 2,844,641 (sawa na dola za Marekani 1,229.1) mwaka 2022 kutoka wastani wa shilingi 2,708,999 (sawa na dola za Marekani 1,173.3) mwaka 2021.


"Hali hii imewezesha nchi yetu kuingia kwenye kundi la nchi zenye kipato cha Kati cha Chini, " Amesema Waziri Jafo. 


MAFANIKIO YA MAZINGIRA


Tangu kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza na kuratibu shughuli ya hifadhi na usimamizi wa Mazingira ili kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali asili na maendeleo endelevu kwaajili ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho. 


Idara ya Mazingira ilianzishwa mwaka 1992 ikiwa ni juhudi za  Serikali kuhimiza uhifadhi na usimamizi wa Mazingira nchini kama ilivyohimizwa na Azimio la Rio mwaka 1992 linalozitaka nchi zote duniani kutambua uhusiano uliopo kati ya maendeleo na mazingira.


Amesema kufuatia kuanzishwa kwa Idara ya Mazingira, Tanzania iliridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohusu Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira, ambapo katika kutekeleza Azimio Rio la Mwaka 1992, Tanzania iliandaa Mpango wa Kwanza wa Taifa wa Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (National Environmental Action Plan  NEAP) mwaka 1994.


Ameeleza kuanzia wakati huo, Sera ya Mazingira ya mwaka 1997, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191, Programu, Mikakati, Mipango na Miongozo mbalimbali ya kitaifa ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira imeandaliwa na kutekelezwa.


Katika utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, jumla ya Sheria Ndogo 326 zimeandaliwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Mikoa ya Dodoma (15), Kilimanjaro (7), Mbeya (57), Mtwara (69), Morogoro (53), Pwani (59) na Ruvuma (66).


Aidha amesema Kuanzia mwaka 2012 hadi sasa takribani vyeti 2812 vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na Vyeti 1534 vya Ukaguzi wa Mazingira vilitolewa kwa Miradi mbalimbali. Vilevile, Vyeti vya Tathmini ya Mazingira Kimkakati 17 vilitolewa kwa ajili ya kuandaa na kutekeleza Sera, Mipango na Miradi ya Kimkakati.



Serikali imeendelea kutekeleza Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997 ambapo mafanikio makubwa yamepatikana katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuratibu utekelezaji wa Kampeni ya Upandaji Miti nchini ambapo kila Halmashauri ya Wilaya imeelekezwa kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI