NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Prof. Patrick Ndakidemi amekabidhi gari la kubeba wagonjwa na baadhi ya vifaa tiba katika Kituo cha Afya Cha Umbwe kilichopo katika Kata ya Kibosho Magharibi, Tarafa ya Kibosho, Jimbo la Moshi Vijijini.
Gari hilo litasaidia kutoa huduma katika Tarafa ya Kibosho yenye jumla ya Kata sita, na zile jirani za Jimbo la Hai.
Mgeni Rasmi katika hafla hiyo ya utoaji wa gari hilo na vifaa tiba alikuwa Mhe. Patrick Boisafi, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro.
Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Abraham Urio, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dr Kweka na Katibu wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya Dr Didas Munishi, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Moshi, watendaji wa serikali, Mhe. Prosper Massawe Diwani wa Kata ya Kibosho Magharibi, Mhe. Fabiola Massawe, Diwani wa Viti Maalumu, viongozi wa CCM Kata ya Kibosho Magharibi, wauguzi pamoja na Wananchi kutoka vijiji jirani.
Akizungumza na wananchi waliohudhuria katika hafla hiyo, Mwenyekiti Boisafi amewataka wananchi kuendelea kuiamini na kuiunga mkono Serikali ya awamu ya sita kwani imesambaza miradi mingi ya maendeleo katika Kata ya Kibosho Magharibi na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.
Amewaomba wananchi waendelee kuwachagua viongozi wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi ili iwe rahisi kuhudumiwa na Serikali iliyoundwa na CCM.
Akitoa salamu zake, Mbunge Ndakidemi ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita kwa jinsi inavyozidi kupeleka huduma za aina mbalimbali karibu na jamii, likiwemo hilo gari la wagonjwa na vifaa tiba ambavyo vimeletwa kituoni hapo.
Mbunge alipata fursa ya kukabidhi miche bora ya migomba kwa mgeni rasmi na wananchi waliohudhuria.
Akitoa shukrani zake, Diwani Massawe amemshukuru Mbunge kwa namna alivyopambana na kuhakikisha wanapata gari la kusafirisha wagonjwa na vifaa tiba kwa ajili ya kata yake kwani lilikuwa hitaji lao kubwa.
Wananchi wa Kata ya Kibosho Magharibi wakizungumza kwa nyakati tofauti wameishukuru Serikali kwa kuwaletea huduma ya gari la wagonjwa kwani lilikuwa hitaji lao la muda mrefu.
Mwisho.
0 Comments