Na HADIJA OMARY
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,Maliasili na utalii chini ya mwenyekiti wake Thimotheo Paul Mzanva (mb) imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada mbalimbali anazozifanya za kukuza Utalii .
Akizungumza mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea hifadhi ya urithi wa utamaduni wa Dunia,magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara na kukagua miradi minne iliyoghalimu kiasi cha shilingi Bilion 1.4,kupitia fedha za Uviko 19 mwenyekiti wa kamati hiyo Thimotheo Paul Mzanva (mb) amesema kamati imeonyesha kulidhishwa na utekelezaji wake .
Miradi hiyo waliyoikagua ni boti ya utalii iliyowezesha kupatikana kwa boti zingine tatu,njia za kutembeza watalii na jengo la kupokelea wageni,na uendelezaji wa gati imara na za kisasa zitakazoweza kupokea meli kubwa za watalii.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mzanva amesema ubora uliopo kwenye miradi hiyo imesaidia kuongeza idadi ya watalii na mapato ambapo amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa za kukuza utalii nchini .
Hata hivyo ametoa wito kwa TAWA na Wizara ya maliasili kuendelea kuongeza juhudi zaidi katika kuboresha miundombinu kwenye eneo hilo la Kilwa Kisiwani pamoja na kubaini vivutio vingine zaidi vya utalii.
Akizungumzia ziara hiyo,Waziri wa Maliasili na utalii Angellah Kairuki amesema Wizara inafurahishwa kwa namna TAWA wanavyolisimamia eneo la Kilwa Kisiwani vizuri ambapo kwa takriban miaka 3 tangu wakabidhiwe eneo hilo wameweza kuliendeleza vizuri kupitia fedha mbalimbali zinazotolewa na Serikali na hivyo kuongeza idadi ya watalii kutoka 2988 kwa mwaka 2018/2019 hadi kufikia Watalii zaidi ya 6000.
Amesema kwa Mwaka huu wa fedha 2023/2024 kwa kipindi cha miezi 7 kuanzia Julai 2023 mpaka Februari 2024 watalii zaidi ya 4030 wametembelea kwenye eneo hilo la Kilwa Kisiwani wakiwemo wandani na idadi hiyo imeendelea kuimarika na kwamba serikali kupitia wizara ya maliasili itaendelea kuwekeza na kuibua vivutio vipya vya utalii.
Eneo la Kilwa Kisiwani na Songo Mnara Mkoani Lindi ni miongoni mwa maeneo 7 yaliyotangazwa na UNESCO kuwa ni maeneo ya Urithi wa Dunia .
0 Comments