Header Ads Widget

WANANCHI UCHAKAVU WA MIUNDOMBINU YA KITUO CHA AFYA MWIKA MSAE...



NA WILLIUM PAUL, Moshi.

WANANCHI wa Kijiji cha Msae Nganyeni kata ya Mwika kaskazini wilaya ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro wamelalamikia uchakavu wa miundombinu ya kituo cha afya Mwika Msae  hali ambayo inasababisha kukosa huduma.


Hayo yalijiri mara baada ya Umoja wa wanawake wa chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Moshi vijijini kufanya usafi na kupanda miti katika mazingira ya kituo hicho cha Afya Mwika Msae na kusherekea miaka 47 ya chama hicho tangu kuanzishwa kwake.



Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi hao walisema kituo hicho cha Afya kimekua na kero mbalimbali ikiwemo ukosefu wa huduma muhimu ya maji, uhaba wa madaktari, watoa huduma ya afya pamoja na uchakavu wa majengo jambo ambalo linawafanya kufuata huduma hiyo mbali.


Grace Ngowi alisema changamoto kubwa inayowakabili wagonjwa hasa wanawake wajawazito ni ukosefu wa maji pamoja na kutopatikana kwa urahisi daktari nyakati za usiku hivyo kuwalazimu kwenda mbali kufuata huduma hiyo



"Kituo chetu hakina maabara hivyo tunalazimika kwenda kupata vipimo hospitali nyingine ndipo sasa tuje tena hapa kuhudumiwa, tunaomba serikali itusaidia sisi wananchi ndiyo tunateseka". alisema Gaspa Renald


Naye Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Heriel alikiri kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo uchakavu wa miundombinu ya majengo, uzio wa kituo pamoja upungufu wa watumishi wa afya, ukosefu wa maji hali ambayo inaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.



Kwa upande wake mwenyekiti wa Umoja wa wanawake CCM wilaya ya Moshi (UWT) Ruwaichi Kaale alisema serikali inatambua umuhimu wa huduma ya afya kwa wananchi wake kwa kuhakikisha inaboresha vituo vyote vya afya ili kuchagiza maendeleo ya taifa kwakua afya ni mtaji wa kwanza, huku akiwatoa hofu wananchi kwamba changamoto hizo ziko mbioni kutatuliwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Samwel Shao ni diwani wa kata hiyo ya Mwika kaskazini wilaya ya Moshi, alisema amekua akifanya jitihada za kuhakikisha maboresho ya kituo hicho cha afya Mwika Msae kinatekelezwa hususani kupitia baraza la madiwani na ofisi ya Mkurugenzi ikapitishwa shilingi milioni 250 kwa ajili ya maboresho hayo lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika.



"Ni kweli wananchi wanapata shida kwa kukosa huduma za afya kwenye kituo hiki, hasa wanawake wajawazito na wodi ya wanaume kutokana na uchakavu mkubwa wa miundombinu, tunaendelea kusisitiza serikali katika vikao ili kituo hiki kiweze kuboreshwa wananchi wapate huduma hapa". Alisema Diwani Shao


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI