Header Ads Widget

WANAJESHI WALIOSHIRIKI VITA UGANDA WAMLILIA RAIS SAMIA KIFUTA JASHO

 





Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA

WANAJESHI wa Tanzania walioshiriki vita vya Uganda kuanzia 1978 hadi1979 wameupongeza Umoja wa Afrika (AU) kwa kuweka sanamu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika makao makuu ya ofisi hizo yaliyopo mji wa Addis Abba nchini Ethiopia.


Mmoja wa wanajeshi hao, Frank Maghoba, akizungumza leo (Februari 19, 2024) na waaandishi wa habari alisema kilichofanywa na AU ni kutambua jinsi Mwl.Nyerere alivyoshiriki katika ukombozi wa bara la Afrika ambaye alitaka bara lote liwe huru ambapo katika kufikia malengo hayo walitumika wanajeshi wa Tanzania kupigana.


Hata hivyo, Maghoba amesema suala la kuwekwa sanamu hiyo linapaswa kwenda sanjali na kuwalipa wanajeshi walioshiriki vita hivyo ambapo ni zaidi ya miaka 40 sasa hawajalipwa haki zao licha ya serikali ya Uganda kuahidi kuwalipa kifuta jasho kutokana na kushiriki vita hivyo.


”Mhe Rais Samia Suluhu Hassan wanajeshi wengi tulioshiriki vita hivyo hususani Uganda na kufanikiwa kumng’oa nduli Idd Amini ambaye alivamia ardhi ya Tanzania hatujalipwa wakati sisi tulikuwa tunafanya kazi hiyo kwa kutii amri ya Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania ambaye ni Rais Julius Nyerere kipindi hicho,” alisema Maghoba.


Maghoba ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam, alisema kila mwaka wanajeshi walioshiriki vita hivyo vya Uganda wamekuwa wakiitwa kwenye ofisi za Wakuu wa Wilaya kujaza fomu za kumbukumbu na kuahidiwa kulipwa jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa.


“Mhe rais wanajeshi wengi wamekufa bila kupata haki yao wakati wanastahiri kupata asante yao kutoka serikali ya Uganda ambayo inadaiwa ilishatoa fedha hizo, nchi zingine zinaheshimu wanajeshi wake hasa waliofanya kazi ya kulinda heshima ya nchi zao,” alisema Maghoba kwa uchungu.


Rais Samia Suluhu Hassani juzi akishiriki uzinduzi wa sanamu hiyo alisema hiyo inadhihirisha mchango mkubwa wa Mwl.Nyerere katika ukombozi,umoja na amani ya Afrika na fahari ya bara la Afrika katika urithi wake mkubwa.


Rais Samia yupo nchini Ethiopia kushiriki mkutano wa 37 wa wakuu wa nchi za Afrika ambao pamoja na mambo mengine unatarajia kujadili kuhusu amani na usalama wa nchi za Afrika.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI